Home Kitaifa Elimu, zana bora ni Muhimu kwa kilimo

Elimu, zana bora ni Muhimu kwa kilimo

Na Neema Kandoro, Mwanza

KUWAWEZESHA wakulima kwa elimu na zana bora kuendeshea kilimo chao ni njia pekee ya kuinua mapato kwenye sekta hiyo ambayo inaajiri watanzania wengi

Hayo yamebainishwa jana kwenye maonesho ya Nane nane Kanda ya Ziwa Magharibi Jijini Mwanza na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo

Wasambazaji wa pembejeo za kilimo walisema elimu ni kitu mhimu kwa wakulima kuwawezesha kujikwamua kwa kupata tija kwani kwa sasa wanapata mavuno madogo.

Wakulima Martin Gervas na Innocent Charles wote toka Misungwi walisema watatumia mbegu bora za kisasa na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani waweze kupata mavuno mengi shambani.

Bwana Shamba toka Kampuni ya Seed-Co Ayubu Bisaga alisema kuwa ili mkulima aweze kupata mazao yenye tija ni lazima apatiwe elimu ya kufahamu mbegu na zana bora za kutumia katika kilimo chake.

Alisema kutokana na utafiti ambao Shirika hilo limefanya na kupata mbegu bora zinazohimili mabadiliko ya tabia nchi zinaweza kumfanya mkulima kupata mavuno mengi.

Bisaga alisema mkulima akifuata kanuni za kutumia mbolea na viuwatilifu kwa kuzingatia ushauri wa maafisa ugani Tanzania inaweza kupata mazao mengi hivyo kuwa na akiba ya vyakula vya kutosha.

Meneja Masoko Kampuni ya Sinoray Makoye Kayanda alisema kuwa kunahitajika kuwepo kwa mfumo rafiki wa upatikanaji wa mikopo ili kumwezesha mkulima kupata zana bora za kuboreshea kilimo chao.

Alisema wakulima wamekuwa wakipata changamoto ya kupata zana bora za kuwafanya kurahisisha kazi zao hivyo umefika muda kwa wizara na wadau wengine wa kilimo kusaidia hali hiyo

“Mnyororo wa kilimo toka shambani mpaka kufikisha mazao nyumbani unatakiwa kuwa rahisi kumwezesha mkulima kutokupoteza mavuno yao” alisema Kayanda.

Afisa Mauzo wa Kampuni ya Simusolar Mkoani Mwanza Salehe Sewando alisema kupatiwa kwa wakulima pampu za sola kwa ajili ya umwagiliaji kutampunguzia gharama za uzalishaji wa mazao yao.

Sewando alisema kuwa katika kumwezesha mkulima kufikia malengo ya kufanya kilimo endelevu kwa njia umwagiliaji wanatoa zana hizo kwa fedha taslimu na kwa mikopo ili mkulima aweze kumudu.

Bwana Shamba toka Kampuni ya Khan Growers Rashid Abdalla alisema kuwa wamemulenga mkulima mdogo wa mazao ya bustani kumfundisha namna ya kutumia eneo dogo kupata mavuno mengi.

Alisema matumizi ya mbolea zinazozalishwa viwandani na mboji ni mhimu kuwezesha mafanikio kwenye sekta hiyo.

Abdalla alisema kuwa maonesho ya mwaka huu yamekuwa na hamasa kwa vijana wengi kufika kujifunza mbinu za kilimo bora.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!