Home Kitaifa ELIMU YA AMALI: NJIA YA KUKUZA UJUZI KWA AJIRA ENDELEVU

ELIMU YA AMALI: NJIA YA KUKUZA UJUZI KWA AJIRA ENDELEVU

Na Magrethy Katengu

Walimu kuanzia shule za msingi hadi vyuo wameshauriwa kujiendeleza kwa kusomea elimu ya amali (vitendo) ili waweze kuwasaidia watoto kuwa na ujuzi wanapomaliza shule za msingi. Lengo ni kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na ujuzi unaowawezesha kujitegemea, kwani vyeti vya digrii bila ujuzi bado havijakidhi mahitaji ya soko la ajira.

Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha VETA Furahika, Dkt. David Msuya, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo, Januari 28, 2025.

Aidha, Dkt. Msuya amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuthamini elimu ya amali ambayo inalenga kumwandaa mwanafunzi kwa vitendo ili kumwezesha kuwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.

Dkt. Msuya ameongeza kuwa juhudi za Rais Samia katika kuunga mkono vijana wanaosomea elimu ya ufundi (VETA) ni za kupongezwa. Ameeleza kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kusaidia vijana hao kwenye shughuli zao za ujuzi, huku pia ikiwahimiza wazabuni wanaopewa tenda za ujenzi kushirikiana na vijana waliomaliza masomo ya ufundi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Msuya amempongeza Rais Samia kwa juhudi zake za kukuza mahusiano na mataifa mbalimbali, ambapo kupitia diplomasia hiyo, Tanzania imeteuliwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa Nishati, Africa Energy Summit, unaoshirikisha marais 25. Mkutano huo ulianza Januari 27, 2025, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umewakutanisha wakuu wa nchi 54 za Afrika, mawaziri wa fedha na nishati, pamoja na viongozi wa Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Jumuiya ya Ulaya, na Jumuiya ya Afrika.

Lengo la mkutano huo ni kujadili mikakati ya kukabiliana na changamoto za nishati na kuchangamkia fursa zilizopo barani Afrika. Moja ya matokeo makubwa ya mkutano ni kupitishwa kwa Azimio la Dar es Salaam, ambalo linasisitiza dhamira ya viongozi wa Afrika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu kwa maendeleo ya bara hili.

Mkutano huu ni fursa kubwa kwa uchumi wetu. Katika siku hizi mbili za mkutano, Watanzania wamenufaika, hususani kupitia huduma za hoteli na shughuli nyingine za kiuchumi,” alisema Dkt. Msuya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!