Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abeid Galusi, amesema kuwa maboresho yaliyofanyika katika eneo la kupokea na kupakua mizigo yamesababisha kupungua kwa muda wa kupokea mizigo kutoka siku 10 hadi siku 3. Amehimiza wafanyabiashara kufuata mizigo yao kwa wakati ili kuepusha mlundikano.
Kauli hiyo imetolewa leo, Januari 15, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara ya viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania waliotembelea Bandari ya Dar es Salaam.
Galusi amesema kuwa mabadiliko hayo yamefanikishwa na uwekezaji uliofanywa na kampuni ya DP World na Adani Ports. Hata hivyo, ameeleza kuwa bado kuna changamoto ya mlundikano wa mizigo kutokana na wafanyabiashara kutochelewesha mizigo yao.
“Uwekezaji umeleta mabadiliko makubwa, muda wa kusubiri mizigo kwenye meli umepungua kutoka siku 10 hadi siku 3. Tunawaomba wateja wetu waje kuchukua mizigo kwa wakati, kwani sasa bandari ina mzigo mwingi,” alisema Galusi.
Aidha, alisema kuwa kiwango cha uingizaji wa mizigo kimeongezeka kwa asilimia 60 kwa nchi jirani na asilimia 40 kwa mizigo ya ndani, huku sehemu kubwa ya mizigo ikielekezwa katika nchi za Congo, Zambia, na Rwanda.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamis Livembe, alisema kuwa ufanisi wa ushushaji wa mizigo bandarini umeimarisha biashara na kuongeza wateja wa kimataifa.
“Kwa sasa, kushusha mzigo bandarini huchukua siku tatu tu, tofauti na hapo awali. Hii inawapa wafanyabiashara fursa ya kuuza na kuagiza mzigo mara kwa mara, tofauti na siku 40 za hapo awali ambapo mzigo ulisuasua,” alisema Livembe.
Livembe aliongeza kuwa ujio wa DP World na Adani Ports umepunguza muda wa meli kusubiri nje ya bandari, hali ambayo awali ilifikia siku 30 hadi 40. “Kipindi cha nyuma, ucheleweshaji huu ulisababisha gharama za kontena kupanda hadi dola za Marekani 8,000, kutoka dola 3,000.”
Kwa upande wake, Meneja wa Uhusiano wa DP World, Elitunu Mallamia, alisema kuwa kampuni hiyo imeongeza ufanisi na kuvunja rekodi kwa kuhudumia meli 27 katika mwezi Desemba pekee.
“Tunatoa wito kwa wateja kuondosha mizigo yao mapema ili kuongeza nafasi ya kuhifadhi mizigo mipya. Kwa mwaka huu, tumefanikiwa kuhudumia kontena milioni moja, tukivuka malengo yetu,” alisema Mallamia.