Na Mathias Canal, WEST-Zanzibar
Serikali imetoa kiasi cha Dola Milioni tano (USD Mil 5) kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo ya Taasisi ya Chuo cha Bahari Zanzibar ambacho ni kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kilichopo katika eneo la Buyu mjini Unguja Visiwani Zanzibar.
Fedha hizo zimetolewa ambapo UDSM imetakiwa kuhakikisha kuwa inatekeleza kwa ufanisi mkubwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kuhusu usimamizi wa mradi wa Benki ya Dunia wenye takribani Trilioni moja.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 9 Julai 2022 wakati akikagua ujenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari-Zanzibar iliyopo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam wakati akiwa katika ziara ya siku moja kisiwani Unguja.
Waziri Mkenda amesema kuwa mradi huo wa mageuzi ya kiuchumi kupitia elimu ya juu una lengo la kuboresha mitaala na miundombinu ikiwemo kujenga kampasi mpya za vyuo vikuu pia unalenga kutoa ujuzi unaotakiwa na soko hasa uchumi wa viwanda.
Prof Mkenda amempongeza Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambaye ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusimamia na kukagua mara kwa mara ujenzi wa maabara ya muda katika chuo hicho kutokana na maaba ya chuo hicho ikiwemo ofisi kuungua mwishoni mwa mwaka jana katika eneo la Malindi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkenda amemtaka Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi ambao ni wasimamizi wa ujenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari-Zanzibar kuhakikisha anafika haraka iwezekanavyo mjini Zanzibar ili kukagua na kuhakikisha dosari zilizopo katika ujenzi wa chuo hicho zinapatiwa ufumbuzi wa haraka.
“Hatutaruhusu Chuo chetu kikuu chochote ambacho kinafundisha wataalamu halafu kisimamie kazi isiridhishe, tunataka kazi ikisimamiwa na chuo chetu chochote iweze kuakisi ule ubora ambao tunatarajia ” Amekaririwa Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amesema kuwa hata kama muda wa usimamizi wa mradi umekwisha lakini mkandarasi anapaswa kuhakikisha kuwa anakamilisha dosari zote zilizopo ikiwemo ubovu wa marumaru.
Amesema kuwa haitokuwa kazi ngumu kwake kufumua uongozi endapo kazi haitaenda vizuri kama ilivyokusudiwa kwa mujibu wa taratibu za ujenzi na makubaliano katika mkataba wa ujenzi.
Kadhalika Waziri Mkenda amesisitiza kuwa wanafunzi wanaosoma kozi zinazohusu uvuvi wanapaswa kufundishwa kwa vitendo na kupewa kazi za mara kwa mara za kwenda baharini kwa ajili ya kujifunza uvuvi kwa vitendo.