Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amewataka Viongozi wa ngazi zote katika Jimbo lake kwenda kwa Wananchi kuwaelezea kuhusu miradi mbalimbali iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 23 Disemba, 2023 wakati wa kikao chake maalum na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM pamoja na Baraza la Wazazi wa Wilaya ya Mbeya Mjini wakiwemo Madiwani.
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imetekeleza miradi mbalimbali nchini hususani katika Jimbo hilo ikiwemo sekta ya Afya, Elimu, Miundombinu kama vile ujenzi wa barabara ya njia nne kwa kiwango cha lami kutokea Igawa hadi Tunduma na zaidi mradi wa maji kutoka mto Kiwira ambao utamaliza changamoto zote za maji katika Mkoa mzima.
Aidha Dkt. Tulia amewataka Wajumbe kuhakikisha wanalinda viti vyote vya CCM kuanzia ngazi ya Mtaa, Diwani, Mbunge na Rais kwani itakuwa ni aibu kupoteza nafasi yoyote kwakuwa miradi mingi iliyokuwa ni kikwazo kwa Wananchi imetekelezwa na Serikali kikamilifu hivyo kujenga Imani kwa jamii.