Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kujiandaa kikamilifu kukabiliana na kudhibiti vitendo vya rushwa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 hususani kuangazia zaidi kwenye matumizi ya mitandao na simu katika kuhamisha pesa za rushwa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Amesema ni muhimu kujizatiti kupambana na vitendo hivyo vya rushwa ambavyo vina madhara makubwa kwa maendeleo ya Taifa kwa kuwa Viongozi wanaochaguliwa kwa njia ya rushwa hawawezi kukemea vitendo vya rushwa, kutatua kero za wananchi pamoja na kusimamia vema miradi ya maendeleo.
Makamu wa Rais amesema lazima viongozi na watumishi wa TAKUKURU kuwa mfano wa kuigwa kwa mienendo mizuri, kufuatilia tuhuma mbalimbali kwa umakini na bila upendeleo. Ameongeza kwamba ni muhimu kufanya maamuzi kwa haki na kutumia madaraka kutatua kero za wananchi kwa manufaa ya umma na siyo binafsi. Makamu wa Rais ametoa wito kwa TAKUKURU kuzingatia kufanya kazi kwa misingi ya sheria, kanuni na taratibu, kujituma na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele ili Taasisi hiyo iwe na ufanisi.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ni vema kuimarisha mifumo ya kuchunguza, kuzuia na kuadhibu wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa mujibu wa sheria. Amesisitiza ofisi zote za TAKUKURU nchini kuunganishwa na mifumo ya TEHAMA pamoja na kuwajengea uwezo na mbinu za kisasa za uchunguzi na uendeshaji wa kesi za rushwa watumishi wa TAKUKURU wanaotekeleza jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa. Amesisitiza suala la watumishi wa TAKUKURU wanaotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kanuni, pamoja na watoa taarifa kutambuliwa na kulindwa wawapo kazini au nje ya kazi, ili kuepuka kuhatarisha maisha yao.
Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa vyombo vya habari kuunga mkono mapambano dhidi ya rushwa kwa kuelimisha jamii, kuandika taarifa za kiuchunguzi ili kufichua vitendo vya rushwa na kusaidia vyombo vya dola kufanya kazi yake. Amesema kitendo cha baadhi ya vyombo vya habari kudaiwa kutumika kupotosha habari au kutoa habari zenye mrengo fulani, kinaweza kuwa na madhara makubwa katika jamii kwa kuikosesha jamii haki ya kupata habari ambazo zinaweza kuwa na manufaa katika mapambano dhidi ya rushwa.
Ametoa wito kwa Mkutano huo kutumika kubuni mbinu na mikakati ya kukabiliana na rushwa katika mahakama za chini, mabaraza ya ardhi, na vyombo vingine vya haki jinai ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao. Ameisisitiza TAKUKURU kutekeleza agizo la kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya wasimamizi wa miradi watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa au ubadhirifu katika miradi iliyobainishwa wakati wa Mbio za Mwenge 2024.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwekeza katika ujenzi wa Taasisi imara za haki jinai ili kupambana na makosa ya jinai ikiwemo rushwa. Amesema Serikali itaendelea kuiwezesha TAKUKURU kwa upande wa rasilimali fedha na rasilimali watu ili kutekeleza wajibu wake wa kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Crispin Chalamila amesema kutokana na uwezeshaji uliyofanywa na Serikali kwa Taasisi hiyo, katika kipindi cha miezi 12 iliyopita kiasi cha shilingi bilioni 18 kimeokolewa kupitia oparesheni mbalimbali za uchunguzi pamoja na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo. Amesema Fedha hizo zilirejeshwa serikalini na nyingine kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kadri ilivyokusudiwa.
Aidha amesema kwa kipindi cha miezi 12, TAKUKURU inajivunia mafanikio ya ushindi wa Jamhuri wa asilimia 75.5 katika kesi zilizotolewa maamuzi ikilinganishwa na asilimia 67.7 ya ushindi wa kesi zilizotolewa maamuzi mwaka 2023.
Ameongeza kwamba TAKUKURU imeendelea na jukumu lake la kuelimisha umma kuhusu madhara ya rushwa na kuhamasisha umma kushiriki mapambano dhidi ya adui rushwa kupitia njia mbalimbali kama vile mikutano, minada, midahalo, semina, warsha, Mbio za Mwenge wa Uhuru, vipindi vya redio, televisheni na machapisho mbalimbali.
Mkutano huo wa siku nne (Tarehe 16 -19 Desemba 2024) unawakutanisha viongozi wa ngazi ya Taifa, Mikoa na Wilaya wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ili kujadili masuala mbalimbali yahusuyo Taasisi hiyo.