Home Afya DKT.MPANGO: MADEREVA WA M-MAMA WATAKIWA KUWAHUDUMIA AKINA MAMA WAJAWAZITO PAMOJA NA WATOTO...

DKT.MPANGO: MADEREVA WA M-MAMA WATAKIWA KUWAHUDUMIA AKINA MAMA WAJAWAZITO PAMOJA NA WATOTO KWA STAHA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na viongozi mbalimbali wakati akiwasili katika Hospitali ya Mount Meru kuzindua Mfumo wa Kurahisisha Usafiri wa Dharura kwa Mama Wajawazito na Watoto wachanga wa M- Mama kwa Mkoa wa Arusha. Tarehe 22 Juni 2023
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Mkuu wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) Balozi Samantha Power wakimsikiliza Anna Kalanju mkazi wa Mbuguni mkoani Arusha aliyetumia mfumo wa M-Mama katika kupata huduma ya kujifungua wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Kurahisisha Usafiri wa Dharura kwa Mama Wajawazito na Watoto wachanga wa M- Mama kwa Mkoa wa Arusha uliofanyika katika Hospitali ya Mount Meru.Tarehe 22 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Uzinduzi wa Mfumo wa Kurahisisha Usafiri wa Dharura kwa Mama Wajawazito na Watoto wachanga wa M- Mama kwa Mkoa wa Arusha uliofanyika katika Hospitali ya Mount Meru.Tarehe 22 Juni 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa madereva wanaoshiriki katika mfumo wa M- mama kuwahudumia akina mama wajawazito pamoja na watoto kwa staha, huruma na upendo pale wanapowasafirisha kutoka katika maeneo mbalimbali kuelekea katika vituo vya afya.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizindua Mfumo wa Kurahisisha Usafiri wa Dharura kwa Mama Wajawazito na Watoto wachanga wa M- Mama kwa Mkoa wa Arusha katika hafla iliofanyika Hospitali ya Mount Meru leo tarehe 22 Juni 2023. Aidha ametoa rai kwa wale wote wanaohusika na usajili wa akina mama wajawazito kuhakikisha wanatekeleza jukumu hilo kwa ufasaha na kuzingatia namba ya dharura ya simu (115) inafahamika kwa kubandikwa sehemu mbalimbali ili wananchi waweze kuifahamu kirahisi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema mfumo wa M-mama utakapoenea nchi nzima utawezesha kutimiza malengo ya kitaifa na kimataifa ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga huku akihimiza elimu kuendelea kutolewa kwa wananchi kwa kuwahamasisha wanawake wanahudhuria kliniki muda wote wa ujauzito na kujifungua katika vituo vya kutolea huduma ya afya.

Makamu wa Rais amesema serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga. Ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na jitihada ya kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za Afya vinavyotoa huduma kamili za dharura na upasuaji ambapo hadi kufikia mwaka 2022 Serikali imeongeza vituo vya Afya zaidi ya 500 kutoka vituo vya Afya 155 mwaka 2017/18 pamoja na kuongezeka vituo vinavyotoa huduma za watoto wachanga (NICU) kutoka 14 mwaka 2018 hadi vituo 165 mwaka 2022.

Vilevile Makamu wa Rais amewasihi wakazi wa Arusha pamoja na mikoa mingine kusajili akina mama wajawazito na kutumia mfumo wa M-mama ili kuwanusuru wao pamoja na watoto. Amesema mfumo huo ni mkombozi mkubwa kwani kwa mkoa wa Arusha tangu uanze kufanya kazi mwezi Aprili 2023 hadi kufikia tarehe 20 Juni 2023 tayari umeshasafirisha jumla ya dharura 607 ambapo Kati ya hizo, asilimia 82 zilikuwa ni dharura za akina mama na asilimia 18 za watoto wachanga.

Makamu wa Rais amesisitiza kuenezwa nchi nzima, Tanzania Bara na Zanzibar utekelezaji wa mfumo wa M- mama na kuwashukuru wadau wa maendeleo wakiwemo USAID, Vodacom Tanzania Foundation na mshirika wake Vodafone Foundation kwa utekelezaji wa Mfumo huo hapa nchini.

Hadi sasa Mfumo wa Kurahisisha Usafiri wa Dharura kwa Mama Wajawazito na Watoto wachanga wa M- Mama unafanya kazi katika Mikoa 16 ya Tanzania Bara (Shinyanga, Lindi, Mtwara, Morogoro, Dodoma, Manyara, Singida, Simiyu, Mwanza, Mara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Mbeya, Songwe na Rukwa) na Mikoa yote 5 ya Zanzibar. Aidha, Mikoa mingine 10 ya Tanzania Bara ambayo ni Katavi, Kigoma, Tabora, Iringa, Njombe, Ruvuma, Kagera, Geita, Pwani na Dar es salaam ipo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji wa mfumo huo na inatarajiwa kuanza utekelezaji kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!