Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Dira 2050 ni muhimu itambue mahitaji ya vijana na kubeba matamanio yao ili kuifanya iwe ya vijana zaidi na kwa ajili ya vijana kwa kuwa ndio kundi kubwa la watu nchini.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Kitaifa kuhusu Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 lililofanyika katika Ukumbi wa Nkurumah – Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Amesema kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 imebainisha wazi kuwa 77.5% ya watanzania ni vijana, ni muhimu Dira na mikakati yake ya utekelezaji ibainishe fursa na changamoto za muundo na mwenendo huo wa idadi ya watu katika Taifa.
Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa makongamano ya kupokea maoni ya kuwezesha utekelezaji wa Dira kujielekeza katika kutatua tatizo kubwa la utegemezi uliopo hivi sasa wa 87.4%, ikimaanisha ni sehemu ndogo tu ya nguvukazi ya Watanzania ndio inayobeba mzigo mkubwa wa mahitaji ya msingi ya kundi kubwa la wategemezi na hivyo kudidimiza kiwango cha Taifa cha kuweka akiba kwa ajili ya kujenga mitaji ya uwekezaji. Pia amesema ni muhimu kuangazia namna bora ya kutumia nguvu kazi kubwa ya vijana kuharakisha maendeleo pamoja na kuweka nguvu kwenye maendeleo ya elimu ya kujenga ujuzi, stadi za kazi, teknolojia na upanuzi wa shughuli zinazovutia vijana, ikiwemo zinazotumia TEHAMA, Sanaa na Burudani, uwezeshaji wa shughuli zinazochipukia na kilimo janja.
Aidha Makamu wa Rais amesema ni muhimu Dira 2050 ibainishe uwezo na fursa kubwa za nchi kwa kuzingatia mahitaji ya ndani na nje ya nchi. Amesema eneo la kutazamwa kwa karibu ni rasilimali kubwa za madini zilizopo nchini na uvunaji wa madini hususan ya kimkakati unapaswa upangwe kwa umakini mkubwa ili kuweza kunufaisha zaidi Taifa, kwa kuweka viwanda vya uchenjuaji wa madini hayo na kutengeneza bidhaa kama betri za magari ya umeme, bidhaa na vifaa mbalimbali vya kielektroniki, sumaku, mitambo ya kufua umeme kutokana na upepo pamoja na vifaa na vipuli vinavyotumika katika vifaa vya kisasa kama ndege na roketi. Amesema ni muhimu kuyafanya madini hayo kutumika kwa ajili ya kujenga uwezo wa ndani katika kutengeneza bidhaa mbalimbali badala ya kuyasafirisha yote kwenda nje.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Dira mpya inapaswa kujielekeza katika kubadilisha mfumo wa uzalishaji katika sekta za kilimo na mifugo ili kuinua tija mara dufu na kuhakikisha kuwa Taifa linanufaika na Uchumi wa Buluu kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za maji.
Pia amesema Dira ya 2050 itapaswa kubainisha kwa undani changamoto kuu za ndani na za nje, pamoja na zile za zamani na zinazoibukia ambazo ni kikwazo kikubwa kwa nchi yetu katika kupata maendeleo haraka. Halikadhalika amesisitiza umuhimu wa kuangazia changamoto zinazoendelea na mpya, ambazo ni pamoja na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na jinsi ya kuendana na kasi kubwa ya maendeleo ya teknolojia duniani, hususan matumizi ya akili mnemba na roboti.
Makamu wa Rais amesema suala la ulinzi na usalama wa Taifa ni muhimu kuangaliwa katika mtazamo mpya kwa kuzingatia mwenendo wa dunia ya sasa. Ameongeza kwamba Dira mpya ikajenga uelewa wa pamoja na misingi ya mikakati endelevu ya kuhakikisha kwamba nchi na mipaka yake, pamoja na watu wake na rasilimali za Taifa vinaangaliwa na kulindwa vema.
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali, wanazuoni, viongozi wa dini, wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu.