Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete anatarajia kuwa Mgeni rasmi katika kongamano la siku moja la Kimataifa la kumbukizi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambapo Mkuu wa Majeshi wa Zimbabwe, Zimbabwe Defence Forces(ZDF), Luteni Jenerali, Anselem Sanyatwe na Naibu Balozi wa China hapa nchini, Suo Peng, ni miongoni mwa wageni mashuhuri 10 watakaozungumza katika Kongamano hilo.
Hayo yamesemwa na Professa, Marcelina CHIJORIGA, Mkuu wa shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere katika mahojiano na gazeti la Uhuru ofisini kwake jana kwamba kongamano hilo litakalofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Alisema wageni hao wawili watawasilisha mawasilisho tofauti ambapo, Jenerali Sinyatwe atawasilisha mada yenye maudhui ya , kesho (11oktoba 2024) atawasilisha andiko katika mdahalo wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere lenye kichwa cha habari “Changamoto na fursa za kuendeleza dira ya Nyerere: Mtazamo kutoka kwa vyama rafiki sita”,
Aliongeza kuwa Naibu Balozi, Peng, atakiwakilisha Chama cha Kikomunisti cha China(CPC) atajikita katika andiko lenye mada ya, “Ujenzi wa Madaraja: Alama isiyofutika ya msaada aliotoa Mwalimu Nyerere kwa vyama vya kupigania uhuru katika uhusiano wa Afrika na duniani’, huku Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Kikwete akiwa mgeni rasmi atakayefungua mdahalo huo.
“Katika mdahalo huu wa kimataifa wa kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ulioandaliwa na Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere hapa Kibaha, ninayofuraha kuwaeleza kuwa jumla ya wazungumzaji tisa kutoka Namibia, Zimbabwe, Jamhuri ya Watu wa China na Tanzania watawasilisha mawasilisho yenye maudhui tofauti juu ya mchango wa Mwalimu Julius Nyerere katika harakati za mapambano ya ukombozi wa bara la Afrika,”
Kwa mujibu wa Professa CHIJORIGA, wengine watakao fanya mawasilisho ni pamoja na Kanali Mstaafu wa JWTZ, Joseph SIMBAKALIA, atakayewasilisha andiko lenye mada ya: Jukumu la Mwalimu NYERERE katika Mapambano ya Ukombozi Afrika, huku Dkt. Charles MUBITA, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama tawala nchini Nambia- SWAPO, akiwasilisha mada yenye maudhui ya, Jukumu la Elimu ya Itikadi katika Kuhifadhi Alama ya NYERERE.
“Kwa ujumla mdahalo wa kumbukizi ya Mwalimu NYERERE utakaofanyika kutokana na uamuzi na maelekezo ya Bodi ya Usimamizi ya shule yenye wawakilishi kutoka vyama sita rafiki vinavyomiliki shule hiyo kwa maana ya MPLA ya Angola, CCM ya Tanzania, SWAPO cha nchini Namibia, ZANU PF cha Zimbabwe, ANC cha nchini Afrika Kusini, FRELIMO cha nchini Msumbiji na Chama cha Kikomusti cha China (CPC) unalenga mosi kuendana na hadhi ya Mwalimu NYERERE kutokana na ukweli kuwa alikuwa mtu wa kimataifa, akiitumikia dunia nzima na kwa maana hiyo mdahalo huu unakwenda kuwa wa hadhi ya kimataifa kikamilifu.
“Mdahalo huu pamoja na kumuenzi Baba wa Taifa lakini pia unalenga kuwaelimisha vijana wa sasa kwa kurejea historia kuwa Tanzania wakati wa harakati za mapambano ya ukombozi wa bara la Afrika iligeuka kuwa makao makuu ya vyama vya ukombozi vya vyote vya barani Afrika ikiwa ni pamoja na vile vya kutoka Angola kama, Angola’s Popular Movement for the Liberation of Angola(MPLA), National Front for the Liberation of Angola(FNLA) na kile kilichokuja kugeuka kuwa kikundi cha waasi cha National Union for the Total Independence of Angola(UNITA),”
Alisema Mkuu huyo wa Shule ya Uongozi ya Julius Nyerere na kuongeza kuwa kwa upande wa Zimbabwe vilikuwepo vyama vya Zimbabwe African National Union(ZANU PF) and her Zimbabwe African Peoples Union (ZAPU PF).
Kwa mujibu wa Professa CHIJORIGA msaada wa Tanzania kwa wapigania uhuru ambao ulifikia hata Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) kwenda mstari wa mbele haukuishia kwa MPLA, FNLA au ZANU)PF) tu bali ulihusisha pia vyama vya kupigania ukombozi vya Afrika Kusini kama African National Congress(ANC), Pan-Africanist Congress(PAC) South African Communist Party(SACP) pia FRELIMO ya Msumbiji.
Zaidi ya wageni 200 kutoka, Afrika Kusini, China, Mozambique, Angola, Zimbabwe, Uganda, Kenya, Ghana, Nordic States, Umoja wa Afrika (AU), Nigeria nk wamethibitisha kushiriki ambapo Mwanasiasa mahiri na Kiongozi wa Serikali Mwandamizi mstaafu, Stephen Wassira, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na Kamati Kuu ya NEC, atawasilisha wasilisho juu ya maono ya Mwalimu Nyerere juu ya Afrika kujitegemea kiuchumi.