Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuwa Wizara itayafanyia kazi maelekezo, miongozo na maoni yaliyotolewa katika uanzishaji, ujenzi na uendelezaji wa Mradi wa Bandari ya Bagamoyo na Eneo Maalum la Uwekezaji (EPZ) kwa ufanisi na kwa wakati.
Waziri Kijaji ameyasema hayo alipokuwa akijumuisha maoni na mapendekezo ya Wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ya Machakato wa Uanzishwaji, Ujenzi na Uendelezaji wa Mradi wa Bandari ya Bagamoyo na Eneo Maalum la Uwekezaji (EPZ), Oktoba 19 2022 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Aidha, Dkt. Kijaji amewaeleza Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kutekeleza jitihada mbalimbali zinazolenga kuendeleza Sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ukiwemo Mradi huo wa kielelezo wa Bagamoyo ili kujenga uchumi shirikishi na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025
Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Daniel Sillo walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha utekelezaji wa mchakato wa uanzishaji, ujenzi na uendelezaji wa Mradi wa Bagamoyo ambao ni muhimu katika kukuza biashara na ujenzi wa uchumi wa taifa kwa haraka na kwa kuzingatia wawekezaji sahihi wenye uwezo wa kuwekeza nchini.
Awali , Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya nje EPZA Bw. Charles Itembe amesema lengo la uendelezaji wa mradi huo ni ujenzi wa Bandari ya kiwango cha kimataifa kama kitovu cha usafirishaji na lango la biashara ya kimataifa inayofungamana na eneo la viwanda kwa ajili ya uzalishaji na uongezaji thamani mazao mbalimbali yanayozalishwa hapa nchini.
Amesema Mradi huo unaotekelezwa Bagamoyo mkoani Pwani unafaida kubwa kwa Taifa ikiwemo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, kukiza teknolojia, ujuzi na ajira, kukuza biashara ya usafiri baharini na faida kwa kampuni wazawa, fedha za kigeni na kuongeza pato la taifa.