Mwandishi wa kitabu Elimu na Malezi kwa Watoto katika Zama za Kidigitali, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Dkt. Haji Mnasi, amezindua kitabu hicho katika kijiji cha Kitangari Sokoni kilichopo wilayani Newala, mkoani Mtwara. Uzinduzi huo umefanyika leo, tarehe 26 Januari 2025, katika viwanja vya mpira vya Shule ya Msingi Kitangari B.
Dkt. Mnasi amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kumuamini. Alisema licha ya kuwa na majukumu mengi ya kiserikali, aliwiwa kuandika kitabu hicho cha Elimu na Malezi kwa Watoto katika Zama za Kidigitali.
“Kutokana na kasi kubwa ya ukuaji wa utandawazi, ambao kwa kiwango kikubwa unaathiri mila na tamaduni za jamii yetu, kitabu hiki kinaenda kuwa suluhisho katikati ya zama hizi za utandawazi na ukuaji wa teknolojia,” alisema Dkt. Haji Mnasi.
Aidha, Dkt. Haji Mnasi amewataka wazazi, walezi, pamoja na jamii kwa ujumla kupata nakala za kitabu hicho ili kuwasaidia watoto kujifunza na kupata elimu pamoja na malezi bora. Lengo kuu ni kukuza taifa lenye maadili mema na uchapakazi, kama ambavyo maono ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan yamejikita katika kusisitiza ujenzi wa jamii bora na kizazi salama cha kesho.