Home Kitaifa DKT.BURIANI ATOA KONGOLE KWA TANZANIA NA UGANDA KUTEKELEZA MRADI WA BOMBA LA...

DKT.BURIANI ATOA KONGOLE KWA TANZANIA NA UGANDA KUTEKELEZA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA

📌 Aeleza faida za mradi mkoani Tanga

📌 Asema EACOP itafungua fursa za tafiti za Mafuta Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Batilda Buriani ameipongeza Serikali ya Tanzania na Uganda kwa kujenga Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ambalo limefungua fursa za uwekezaji kwa wakazi wa Nchi hizo mbili zenye mahusiano mazuri kwa muda mrefu.

Amesema mahusiano hayo ndio yamepelekea Tanzania kuwa mdau mkubwa katika ujenzi wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi ambapo mkoa wa Tanga utapokea mafuta hayo kutoka Uganda na kuyasafirisha kwenda nje ya nchi.

Ametoa kauli hiyo Novemba 9, 2024 wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa Mradi huo wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga ikiwemo Chogoleani ambapo miundombinu ya kupokea mafuta inajengwa.

“Mkoa wa Tanga kwa upande wa Tanzania ndio sehemu ya mwisho katika mradi ambapo mafuta yatahifadhiwa kwa muda kabla ya kupelekwa kwenye meli kubwa ili yasafirishwe, pia ujenzi wa matanki umefikia asilimia 65 ambapo ujenzi wa mradi umefikia asilimia 45.5.” Amesema Dkt.Buriani

Ameeleza kuwa, Mradi huo wa kimkakati ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa utatue changamoto ya ajira hasa kwa Vijana.

Amesema mradi huo umeongeza msukumo kwa vijana kusoma katika vyuo vya ufundi ili waweze kupata fursa za ajira..

Ameongeza kuwa, Wilaya sita katika Mkoa wa Tanga zimepitiwa na mradi ambazo ni Handeni, Muheza, Kilindi, Korogwe, Mkinga na Tanga ambapo fidia ya gharama ya ardhi katika baadhi ya maeneo ambapo mradi unapita imeanza kulipwa.

Pia kambi za wafanyakazi zinajengwa pamoja na kambi za kupunguza msukumo wa mafuta kwa kuwa yatakuwa yamefika mwisho kutoka Uganda na kupita baadhi ya mikoa ya Tanzania ili kuweza kuhifadhiwa kwenye matanki makubwa kabla ya kupakiwa kwenye Meli za mafuta kwenda mataifa ya kigeni.

Amesisitiza kuwa, Mradi huo utaifungua Tanga kwa kuwa kuna tafiti za kutafuta mafuta zinaendalea kufanyika katika maeneo ya nchikavu na baharini, aidha mkoa wa Tanga ndio wenye miundombinu mikubwa ya kuhifadhi Mafuta Ghafi hapa nchini.

Dkt. Buriani amesema kuwa Mradi unazingatia uhifadhi wa mazingira katika maeneo yote ya Bahari na shughuli za kijamii ikiwemo Elimu ya Kilimo, Usalama barabarani kwa makundi maalum, huduma za kijamii pamoja na kukuza kipato cha kaya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!