Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameikataa taarifa ya Mgodi wa Geita Gold Mine Limited (GGML) ambayo haijabainisha mahitaji ya ardhi katika leseni yake na hatma ya watu wanaoishi ndani ya vigingi katika leseni ya mgodi huo.
Dkt. Biteko ameikataa taarifa hiyo iliyowasilishwa na Makamu wa Rais wa Kampuni ya AngloGold Ashant inayomiliki mgodi huo Simon Shayo katika kikao kilichofanyika mkoani Geita ili ichakatwe upya kwa lengo la kujibu changamoto za wananchi wa Geita.
Kampuni ya AngloGold Ashant iliahidi kuwasilisha taarifa itakayotoa suluhisho la kudumu la changamoto ya kulipa fidia kwa wananchi wa Geita ili kupisha maeneo ya uwekezaji katika mgodi huo au kuendelea kuishi katika maeneo yao na kuyaendeleza ambapo taarifa hiyo haijaeleza masuala hayo.
Amesema malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Geita wanaoishi ndani ya vigingi kwenye leseni ya mgodi wa GGML ambao wananchi wanatakiwa kulipwa fidia ya maeneo yao ili kupishe uwekezaji au kuendelea kuishi na kuyaendeleza maeneo yao inapaswa kufika mwisho na kujulikana hatma ya changamoto hiyo.
“Katika taarifa ya GGML nilitarajia kusikia changamoto ya watu wanaoishi ndani ya vigingi vya leseni ya mgodi wanalipwa fidia au wanaachiwa maeneo yao lakini taarifa hii haijazungumzia hilo,” amesema Dkt. Biteko.
Kufuatia hatua hiyo, Dkt. Biteko amesema hadi kufikia Januari 09, 2023 mgodi huo uwe umewasilisha taarifa inayojibu changamoto zinazotakiwa kupatiwa majibu na hatma ya watu wanaoishi ndani ya vigingi vya mgodi huo ijulikane.
“Watu wanaoishi ndani ya vigingi vya mgodi wa GGML wameambiwa wasiendeleze maeneo yao, sasa wanalipwa fidia au wanaachiwa maeneo yao ili waendelee na maisha yao ikiwemo kuyaendeleza maeneo yao,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko ameutaka mgodi wa GGML kuichakata upya taarifa hiyo ili iweze kuwa na majibu ya hatma ya watu wa Geita ambao wameteseka kwa muda mrefu ili Wizara itoe muelekeo maalumu juu ya hatma ya jambo hilo.