Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa maeneo yaliyopo kwenye hifadhi bado yanatafutiwa ufumbuzi ili wachimbaji wa madini waweze kuchimba na kunufaika na rasilimali hizo.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Julai 1, 2022 alipotembelea na kuzungumza na wachimbaji wadogo katika eneo la Lugelele wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya katika ziara yenye lengo ya kukagua shughuli za uchimbaji madini na kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji hao wa madini ya dhahabu.
Ameongeza kuwa, Serikali inayatafutia ufumbuzi maeneo yaliyopo kwenye hifadhi ili kuwawezesha wachimbaji na hivyo kunufaika na rasilimali madini.
Amefafanua kuwa, maeneo yaliyopo chini ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA) bado hayaruhisiwi kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo mpaka sasa. Aidha, kwenye hifadhi za misitu amefafanuwa kuwa, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) haijazuia shughuli za uchimbaji madini.
“Maeneo ya hifadhi ya wanyamapori hakuruhusiwi shughuli za kibinadamu, za uchimbaji madini zinazoruhusiwa ni za aina mbili tu, kutafiti mafuta na gesi na kuchimba madini ya nishati,” amesisitiza Dkt.Biteko.
Ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anataka kuwaona wachimbaji wanapewa fursa kwenye uchimbaji wa madini ili waweze kunufaika na rasilimali madini.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune amesema kuwa, shughuli za uchimbaji madini katika wilaya hiyo zimekuwa fursa kwa wananchi katika kujipatia kipato cha kila siku.
Amesema, wachimbaji wengi wanapata ajira katika maeneo hayo na amemweleza Waziri Biteko kuwa, wilaya ya Mbarali inapata wastani wa kilo 2.5 ya dhahabu ambayo huchangia kwenye Pato la Taifa na halmashauri hiyo.
Katika hatua nyingine Dkt. Biteko ametembelea kiwanda cha kuzalisha kokoto cha TAZARA Kongolo Quarry ili kujionea shughuli zinazofanyika katika kiwanda hicho.