Na Shomari Binda-Musoma
DIWANI wa viti maalum manispaa ya Musoma Asha Muhamed ametoa swadaka ya mkono wa Eid el Fitr kwa wanafunzi na watu wenye uhitaji.
Asha amewafikia wanafunzi wa shule ya wasichana Songe na shule ya ufundi Musoma pamoja na wagonjwa waliopo hospitali ya manispaa Musoma pamoja na sikukuu ya Eid na iftar ya kumalizia mwezi mtukufu was Ramadhan.
Akizungumza kwa nyakati tofauti kwa wale aliowafikia amesema mwezi mtukufu wa Ramadhan ni mwezi wa baraka na swadaka ni bora zaidi kutolewa kwa wahitaji.
Akiwa shuleni Songe mara baada ya kukabidhi swadaka amewasihi wanafunzi wa kike kumtanguliza Mungu kwenye masomo yao na kuzingatia walimu wanacho kifundisha.
Amesema elimu ndio msingi wa maisha na wasikubali vishawishi vitakavyokatisha ndoto zao za hapo baadae.
Diwani huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam mkoa wa Mara amewaambia ili kila mmoja kuweza kufikia ndoto yake anapaswa kuishika elimu.
“Watoto wangu leo nimewatembelea kuwaletea swadaka ta iftar na mkono wa Eid el fitr lakini kuja kukumbushana umuhimu wa elimu.
“Kubwa tusikubali vishawishi vitakavyoweza kukatisha ndoto zenu na kile kilichowaleta hapa shuleni”,amesema
Akizungumza na wagonjwa kwenye hospitali ya manispaa ya Musoma amesema kuugua ni ibada na wanapaswa kumshukuru Mungu kwa kila jambo
Diwani huyo katika swadaka yake amekabidhi mchele,mafuta,sukari,maharage pamoja na nyama ya ng’ombe
Wakati huo huo kiongozi huyo kwa upande mwingine kama kiongozi wa dini ameshiriki makabidhiano ya ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara hii leo