Na Shomari Binda-Musoma
DIWANI wa viti maalum manispaa ya Musoma na mjumbe wa kikundi cha wanawake wa kiislam Istiqama Asha Muhamed ameongoza utoaji msaada kituo cha malezi kwa watoto.
Msaada huo wa mafuta ya kujipaka,sabuni,unga wa ngano,juice na vitu vingine vimetolewa na kikundi hicho kwenye kituo cha Musoma Home Children’s kilichopo Bweri manispaa ya Musoma.
Akizungumza na Mzawa Blog diwani Asha amesema wanawake wa kiislam kupitia kikundi cha Istiqama wameamua kwenda kuwapa faraja watoto hao walio na umri chini ya miaka 5 wanailelewa kituoni hapo.
Amesema watoto hao wengi wao walitelekezwa na wazazi wao mara baada ya kujifungua hivyo wanahitaji kupewa faraja.
Asha amesema jamii inapaswa kuwa na moyo wa upendo na kujitoa kusaidia wenye uhitaji kwenye maeneo yao.
” Wana kikundi cha wanawake wa kiislam Musoma mjini kwa michango yetu kwa pamoja tumepata mahitaji na kuamua kuja kuwasaidia watoto hawa.
” Jamii inapaswa kuguswa na kujitoa kusaidia wenye uhitaji wakiwemo watoto wadogo wa kituo hicho”,amesema.
Kwa upande wake katibu wa kikundi hicho Bahati Issa amewashukuru wana kikundi hao kwa michango yao na kufanikisha zoezi hilo la mkono wa faraja.
Mmoja wa walezi wa watoto hao Paulina David ametoa shukrani kwa wanawake wa kikundi cha Istiqama kwa kuwakumbuka na kuwasaidia watoto.