Home Kitaifa DC UKEREWE AMEAGIZA UJENZI WA BWENI NA BWALO UKAMILIKE KWA WAKATI.

DC UKEREWE AMEAGIZA UJENZI WA BWENI NA BWALO UKAMILIKE KWA WAKATI.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mkoa wa Mwanza Mhe. Hassan Bomboko ameagiza mradi wa ujenzi wa bweni na bwalo katika Shule ya Sekondari Bwiro na Ilangala kuwa miradi hiyo ikamilike kwa wakati uliokusudiwa, pia amehimiza wazazi kupeleka watoto waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2023 katika shule zao.

“Rai yangu katika kuutunza mradi huu, fedha nyingi zimetumika katika uwekezaji, kwenye eneo la Elimu ambayo ndiyo agenda yetu mama na kwa kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan amewekeza fedha nyingi ningependa kuona viongozi wote tukishirikiana kuitunza miradi hii ili isaidie vizazi vijavyo” amesema Mhe. Bomboko.

“Nitumie fursa hii kukupongeza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Emmanuel Sherembi na viongozi wengine wote kwa juhudi kubwa mliyoifanya katika kusimamia ujenzi wa miundombinu hii, nimejiridhisha miradi ipo vizuri, tujitahidi kukamilisha pale ambapo hapajakamilika ili ndoto ya Rais wetu itimie ya wanafunzi kulala bweni na kusomea katika vyumba vya madarasa bora.” amesema Mhe. Bomboko.

Akisoma taarifa ya utekelezaji miradi ya TASAF Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ukerewe Bi. Jenista Damaseni ameeleza kuwa Wilaya ya Ukerewe ilipata fedha kutoka ufadhiri wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC – Organization of the Petroleum Exporting Countries) kwa kuandika maandiko mradi ambayo yalihudisha miradi 15.

Bi Damaseni ameeleza kuwa jumla ya Shilingi Millioni 378, 206, 352.84 zililetwa 04.04.2022 ambapo utekelezaji wake ulianza 17.05.2022 na awamu ya pili kiasi cha Shilingi Millioni 446, 869, 926.77 zilizoletwa katika Halmashauri hiyo 24.10.2022 na utekelezaji wake kuanza 15.11.2022, amefafanua kuwa utekelezaji wa mradi ulitakiwa nguvu ya wananchi 10% ambapo ni sawa na Millioni 30.8 likiwa ni takwa la mradi ikijumuisha kusomba mchanga, kujaza vifusi, maji, kuchimba msingi na kusogeza vifaa mbalimbali ikiwemo tofari.

Aidha, Bi Damaseni ameitaja miradi iliyopata fedha awamu ya kwanza kuwa ni ujenzi wa bweni moja Shule ya Sekondari Bwiro, Ujenzi wa bwalo Shule ya Sekondari Bwiro, ukarabati wa barabara Musomi hadi Irundu Km 2.0 ujenzi upo katika hatua ya ukamilishaji.

“Fedha iliyotolewa awamu ya pili imetekeleza ujenzi wa Bwalo 1 katika Shule ya Sekondari Ilangala, ujenzi wa Bweni 1 Shule ya Sekondari Ilangala, pia ujenzi wa madarasa mawili 2, vyoo matundu 4 ya wanafunzi na matundu 2 ya Walimu ikiwa pamoja na thamani zake, ujenzi mwingine ni vyumba viwili vya madarasa, matundu 4 ya vyoo vya wanafunzi na matundu 2 ya vyoo vya Walimu.” amesema Damaseni.

Akifafanua changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi Bi. Damaseni ameeleza kuwa kupanda kwa bei za vifaa pamoja na huduma tofauti na gharama zilizo kwenye andiko mradi ni moja ya changamoto ambayo imejitokeza katika utekelezaji huo.

Nae Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ukerewe Mhe. Ally Mambile amepongeza ujenzi pamoja na kamati za ujenzi katika maeneo yote ya miradi iliyofikiwa na ziara hiyo, amesisitiza wazazi kuwapeleka watoto shule ili kupata Elimu ikiwa ni malengo ya serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!