Mkuu wa Wilaya ya Same, Kaslida Mgeni, amewaasa wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mtaa, huku akisisitiza kuwa wananchi wasikae kwenye vituo vya kupigia kura baada ya kumaliza kupiga kura.
Kaslida aliyasema hayo leo, Novemba 27, wakati alipojitokeza kupiga kura katika Kituo cha Stesheni, Kata ya Stesheni, wilayani Same, na kusema kuwa kupiga kura ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania.
“Hatutegemei kuona wananchi wanakaa kwenye vituo vya kupigia kura baada ya kumaliza. Wanapaswa kurudi nyumbani na kusubiri matokeo yatakapotangazwa. Mimi nimeshapiga kura, nimetimiza wajibu wangu wa kikatiba tayari,” alisema Kaslida.
Akiendelea na maelezo yake, Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa zoezi la uchaguzi katika Wilaya ya Same linaendelea vizuri, huku akisisitiza kuwa usalama umeimarishwa. Aliwataka wananchi ambao bado hawajafika kwenye vituo vya kupigia kura kujitokeza kwa wingi na kutumia haki yao ya kidemokrasia.
“Uchaguzi huu utakuwa wa haki na utazingatia demokrasia. Atakayeshinda atatangazwa kama mshindi,” alifafanua Kaslida.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupiga kura walieleza kuridhishwa na utaratibu wa uchaguzi na kusema ni jambo la kihistoria litakalosaidia kuleta maendeleo katika mitaa yao. Rashid Mussa, mmoja wa wapiga kura, alisema: “Nimeshapiga kura na Serikali imefanya kazi kubwa. Imeonyesha ukomavu wa kidemokrasia na kutoa elimu muhimu kwa wananchi. Niwaombe wenzetu waliopo majumbani wajitokeze na kupiga kura.”
Uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mtaa hufanyika kila baada ya miaka mitano, na ni haki ya kikatiba kwa kila Mtanzania kuchagua kiongozi anayeendana na matakwa yao.