Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amezindua kampeni ya tamasha la utalii awamu ya pili, “Same Utalii Festival”, ambalo litarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 20 hadi 22 Disemba 2024. Tamasha hili litafanyika katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, na linatarajiwa kuvutia umati mkubwa wa wageni.
Katika uzinduzi uliofanyika katika hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Mheshimiwa DC Kasilda alieleza kuwa lengo kuu la tamasha hili ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kutangaza vivutio vya utalii nchini kupitia filamu maarufu, “Tanzania the Royal Tour”.
Kasilda aliongeza kuwa tamasha hili ni fursa muhimu kwa Wilaya ya Same, kwani linatarajiwa kuleta uwekezaji mpya katika sekta ya utalii na kuongeza ajira kwa wananchi. Aidha, tamasha hilo litasaidia kutangaza utalii wa asili, hususani tamaduni za kabila la Wapare na Wamaasai, ambao ni sehemu muhimu ya utamaduni wa eneo hili.
Mkuu wa Wilaya hiyo alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika tamasha, akisema, “Tamasha lililopita limeibua fursa nyingi za ajira, hususan kwa wamiliki wa hoteli na wajasiriamali. Tunatarajia tamasha hili litakuwa na mafanikio makubwa zaidi.” Pia aliwataka wananchi kujitokeza kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kuimarisha uandikishaji wa wapiga kura.
Wadau wa utalii, akiwemo mhifadhi Mkuu wa hifadhi ya Taifa Mkomazi, walionesha matumaini makubwa ya kupokea wageni wengi zaidi mwaka huu. Walisema kuwa tangu tamasha la kwanza, idadi ya watalii imeongezeka kutoka 7,000 hadi zaidi ya 20,000, wakiwa na matumaini makubwa ya ongezeko la wageni.
Tamasha la mwaka huu litajumuisha matukio mbalimbali ya utalii, safari ya treni kutoka Dar es Salaam hadi Same, na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali. Linatarajiwa kuwa tamasha kubwa zaidi kuliko la mwaka jana, likilenga kuimarisha sekta ya utalii katika Wilaya ya Same.
Tamasha la “Same Utalii Festival” linatoa fursa si tu kwa wajasiriamali, bali pia kwa jamii nzima, kuonyesha utajiri wa utamaduni na vivutio vya asili vilivyopo katika eneo hili la kipekee.