Na Ashrack Miraji Same kilimanjaro
Hatimae mawasiliano ya barabara baina ya wakazi wa Kisiwani-Maore, Ndugu,Kihurio na Bendera wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro yamerejea baada ya wakala wa Barabara nchini kufanikisha matengenezo ya Daraja Kihurio lililokuwa limeharibiwa vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo.
Mkuu wa wiaya ya Same Kasilda Mgeni akiwa na kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo ametembelea maeneo yaliyo athiriwa ambapo ameeleza kurithishwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na TANROAD kufanya kazi usiku na mchana kurejesha mawasiliano kwenye eneo hilo.
“Pamoja na kamati yangu ya usalama Wilaya tumeshuhudia daraja limekamilika na Magari yanaendelea na safari zake, niwapongeze wote walioshiriki kuhakikisha mawasiliano yanarejea kwa haraka kama nilivyo elekeza siku Ile ilipotokea dharula”. Alisema Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni.
Pamoja na uharibifu wa miundombinu ya barabara, Mvua hizo zilisababisha pia mafuriko kwenye maeneo mengi ya Wilaya ya Same ikiwa ni pamoja na kuharibu miundombinu ya Skimu za Umwaligiaji maeneo ya kata za Ndugu, Maore na Kihurio ambako ni maarufu kwa kilimo cha mpunga.
Kuna uharibifu pia wa miundo mbinu ya Maji, baadhi ya Nyumba kubomoka wakazi wake wakiachwa bila makazi, ambapo Kwa mujibu wa mkuu wa Wilaya Serikali inaendelea na utekelezaji wa hatua za haraka kurejesha hali ya awali kwenye upatikanaji wa huduma.