Ashrack Miraji Same Kilimanjaro
Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni amewataka wawekezaji wa Madini ya Gypsum (JASI) Makanya kushirikiana na Halmashauri pamoja na Afisa Madini Mkoa wa Kilimanjaro kuanzisha ushirika wa wawekezaji wa Madini ya JASI Same ambao utawasaidia kuweza kuwa na usimamizi mzuri ili uwekezaji wao wanoufanya uweze kuwa na tija kwao na Wananchi wa Same.
DC Kasilda amezungumza hayo kwenye kikao chake na Wawekezaji hao kilichofanyika Kata ya Makanya chenye lengo la kutafuta suluhu ya changamoto wanazokabiliana nazo Wadau wa JASI, ambapo amesisitiza masuala ya ushirikiano baina ya wawekezaji na jamii kwenye maeneo husika hasa kwenye shughuli za maendeleo ili kuleta ustawi mzuri.
Aidha amesisitiza pia Wawekezaji kuzingatia sheria ya utunzaji wa Mazingira baada ya kuchimba Madini ikiwemo kufukia mashimo na kupanda miti lengo ni kudhibiti athari za uharibufu wa mazingira zinazoweza kujitokeza siku za mbeleni lakini pia kuwezesha ardhi hiyo kuwa na matumizi mengine endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Pia amesisitiza Wawekezaji masuala ya CSR ,na Tozo mbalimbali Wahakikishe wanalipa kuanzia ngazi ya kijiji , Halmashauri , TRA na Wizara ya madini.