Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amekutana na wadau wa biashara ya mbao kujadili maendeleo na changamoto zinazowakumba ili ziweze kutatuliwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kukuza uchumi wa wilaya.
Kikao hicho kimefanyika leo, Februari 6, katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Same. Kimewakutanisha wadau mbalimbali wilayani humo, wakiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu Tanzania (TFS), pamoja na viongozi wengine wa serikali. Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kasilda amesisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha biashara ndani ya wilaya inastawi.
“Wafanyabiashara wa mbao ni wadau muhimu, na serikali inawatambua kupitia kodi wanazolipa. Ni lazima tuhakikishe tunaondoa vikwazo vinavyokwamisha biashara zenu ili ziweze kukua. Endapo mnakumbana na changamoto, ni muhimu kutoa taarifa mapema ili tuweze kuzitatua,” amesema Mhe. Kasilda.
Wadau wa biashara ya mbao, wakiwemo wavunaji wa miti na wauzaji wa mbao, wamewasilisha changamoto zao, ikiwemo mzigo wa kodi mbalimbali wanazotozwa kuanzia ngazi ya kijiji. Wataalam husika walipata fursa ya kutoa ufafanuzi kuhusu masuala hayo.
Katika kikao hicho, pia ulijadiliwa umuhimu wa uhifadhi wa misitu kwa maendeleo endelevu ya biashara ya mbao. Wadau waliomba kuwe na uwazi zaidi katika utoaji wa vibali vya uvunaji wa miti ili kuepusha urasimu na ucheleweshaji ambao huathiri biashara zao.
Baadhi ya wafanyabiashara walieleza kuwa kikao hicho kimekuwa na manufaa kwao kwani kimetoa mwanga kuhusu masuala ya kodi na vibali vya biashara. “Tunashukuru kwa fursa hii ya kujadili changamoto zetu moja kwa moja na serikali hii ni hatua bora ambayo imefanyika. Tunaamini mazungumzo haya yatawezesha biashara yetu kukua na kutuletea maendeleo,” amesema Amos Mbwambo, mmoja wa wafanyabiashara wa mbao wilayani Same.
Kwa kumalizia, Mhe. Kasilda amewataka wafanyabiashara kushirikiana na serikali kuhakikisha biashara zao zinafuata sheria na taratibu, huku akihaidi kuwa vikao vya aina hii vitaendelea kufanyika ili kuboresha mazingira ya biashara katika wilaya ya Same.