Home Kitaifa DC SAME AKERWA NA USIMAMIZI HAFIFU MRADI WA UJENZI WA SHULE MPYA...

DC SAME AKERWA NA USIMAMIZI HAFIFU MRADI WA UJENZI WA SHULE MPYA YA AMALI,

Na Ashrack Miraji Mzawa Media

Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Amali iliyopo kata ya Kihurio na kubaini kuwa hakuna maendeleo yoyote katika ujenzi huo kwa zaidi ya wiki tatu huku sababu kubwa ya kusimama kwa ujenzi huo ni ukosefu wa vifaa vya ujenzi, hali iliyowalazimu mafundi kusitisha kazi.

Kutokana na hali hiyo, Mhe. Kasilda ameagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kuhamia eneo la mradi wa ujenzi wa Shule hiyo mara moja ili kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa haraka na kazi kuendelea bila kuchelewa.

Mkuu wa Wilaya huyo ameonyesha kutoridhishwa na usimamizi wa ujenzi wa mradi huo, hasa ikizingatiwa kuwa Januari 14 alifanya ziara shuleni hapo na kubaini changamoto kama hizo, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa licha ya kutoa maagizo.

Mafundi walioko katika ujenzi huo wamemweleza mkuu wa wilaya kuwa wamekuwa wakisubiri vifaa kama mawe, mbao, bati na vifaa vingine kwa zaidi ya wiki tatu bila mafanikio, Wamesema kucheleweshwa kwa vifaa hivyo kunawafanya kupoteza muda mwingi pasipo kufanya kazi yoyote, jambo ambalo likiendelea, wakalazimika kusitisha mkataba wao.

Mhe. Kasilda ameonyesha masikitiko yake juu ya uzembe wa baadhi ya wataalamu wa halmashauri katika kusimamia mradi huo, akisisitiza kuwa fedha zote za ujenzi zilishatolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu mwaka jana 2024.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same kuhakikisha usimamizi unaboreshwa, na ujenzi unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa ili thamani ya fedha zilizotolewa iendane na thamani ya mradi unaotekelezwa.

Shule hiyo ya ufundi inajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 584 na inatarajiwa kuwa mkombozi kwa vijana wa eneo hilo, kwani itawapatia ujuzi wa fani mbalimbali, hivyo kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa mara baada ya kuhitimu masomo yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!