Na WazoHuru Media, Iramba
Ili kuwakutanisha vijana pamoja kwa ajili ya kuimarisha afya zao, kutambua vipaji na kuviendeleza Wilaya ya Iramba imejipanga kuanza mashindano ya mpira miguu.
Mashindano hayo yanayoratibiwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Mhe Suleiman Mwenda yanatarajiwa kuanza mapema mara baada ya msimu wa kilimo kumalizika.
DC Mwenda amebainisha hayo jana tarehe 13 Januari 2023 wakati akizingumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya WazoHuru Media Group Limited Ndg Mathias Canal aliyemtembelea ofisini kwake Mjini Kiomboi.
DC Mwenda amesema kuwa Ligi ya mpira wa miguu ambayo ina lengo la kuimarisha sekta ya michezo Wilayani hapo na kuwakutanisha vijana itasaidia kutengeneza mahusiano imara na madhubuti katika msingi wa maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na Wilaya kwa ujumla wake.
DC MWENDA amewasihi wananchi na wadhamini mbalimbali kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha dhamira hiyo katika kuimarisha sekta ya michezo na kufanikisha kuanza na kumalizika kwa mashindano hayo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya WazoHuru Media Group Limited Ndg Mathias Canal amempongeza DC MWENDA kwa kujipanga kuanzisha mashindano hayo ambayo yatakuwa chachu ya kuitangaza Wilaya ya Iramba na sekta ya uwekezaji.
Amesema kuwa Wilaya ya Iramba ina maeneo mengi mazuri na ardhi ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya Kilimo, Elimu, Mifugo na Uvuvi ikiwa ni pamoja na sekta ya Viwanda.
MWISHO