Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhe. Jerry Muro pamoja na wataalamu wa ardhi kutoka ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri leo tarehe 29/07/2022 wamelazimika kukutana na baadhi ya wananchi wa vijiji vya ulyampiti kata ya UNYAHAATI na mwau kata ya Mang’onyi pamoja na baadhi ya wananchi waliowekeza kwenye shamba la pamoja la kilimo cha korosho lenye hekari elfu tatu
Mhe. Muro ambae amelazimika kutoa ufafanuzi wa Mgogoro wa mpaka wa vijiji hivyo na kusema kwa mujibu wa vipimo vya kitalaamu eneo lenye hekari elfu tatu liko kijiji cha ulyampiti na si vinginevyo
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi ambao waliomba kwa maandishi kupitia kijiji cha mwau kukaa kwenye maeneo hayo wasiondolewa na uongozi wa ulyampiti kwani changamoto imesababishwa na viongozi wa kijiji cha mwau kutokufuata utaratibu hivyo wananchi waliopewa kwa MAANDISHI maeneo hayo kubaki walipo na wasisumbuliwe
Hata hivyo Mhe. Muro amewataka wananchi waliovamia maeneo hayo na kuyatumia pasipo kuomba katika kijiji chochote wawe wameondoka ndani ya siku 30 kuanzia sasa na kuwapisha wananchi waliolipiwa maeneo hayo kwa ajili ya kilimo cha korosho ambapo tayari halmashauri ya kijiji cha ulyampiti wameshakusanya zaidi ya milioni 51 kutoka kwa wananchi wanaotaka kuwekeza kwenye kilimo cha pamoja cha korosho
Akihitimisha mgogoro huo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe. Jerry Muro amesema kwa mwananchi yoyote anaetaka kuishi kwenye eneo hilo la mradi lazima aombe kwa maandishi na awe tayari kulipia gharama za kupewa ardhi na uongozi wa kijiji cha ulyampiti na si vinginevyo
Katika hatua nyingine Mhe.Muro amewaonya baadhi ya wananchi na viongozi kutoka kijiji cha mwau kuacha tabia ya kuvamia mashamba hayo na kuchoma moto mikorosho iliyopandwa na wananchi wanaowekeza katika eneo hilo na kusisitiza hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuchoma miti ya korosho inayopandwa.