Na Gideon Tanga
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Kubecha, amesema pambano la ngumi litakalofanyika jijini Tanga tarehe 16 mwezi huu, linatarajiwa kuwa la kihistoria na litachangia pakubwa kukuza mchezo wa ngumi na vipaji vya mabondia katika mkoa huo na nchini kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kubecha alisema Mafia Boxing Promotion wamekuwa wadau muhimu katika kukuza mchezo wa ngumi, hasa hapa Tanga na Tanzania kwa jumla. Aliendelea kusema kuwa, baada ya kupokea wazo la kushirikiana na wadau hao, alikubaliana kuandaa pambano hili kubwa katika mkoa wa Tanga.
“Kama mkoa, Tanga ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa hamasa ya mchezo wa ngumi. Hivyo, niliona ni muhimu kushirikiana na Mafia Boxing ili kuleta pambano hili hapa Tanga. Tunatarajia mabondia wa kimataifa na wa hapa nyumbani kushiriki,” alisema Kubecha.
Mhe. Kubecha alisisitiza kuwa pambano hili si tu litakuwa la kivutio kwa wapenzi wa mchezo wa ngumi, bali pia litakuwa fursa ya kipekee ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kauli mbiu ya pambano hilo ni: “Ngumi yangu, Uchaguzi wangu, Maendeleo yangu.”
“Kwa niaba ya serikali, tunatoa wito kwa wakazi wa Tanga na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kuungana na mabondia wetu. Pambano hili linalenga kuwa la kihistoria na litatoa fursa ya ajira kwa vijana wetu,” aliongeza Kubecha.
Aidha, alithibitisha kuwa serikali imejipanga vilivyo kuhakikisha usalama wa wananchi na wapenzi wa mchezo. “Tunataka kila mtu aje kwa amani na furaha. Ulinzi utakuwa wa kutosha na familia zinaweza kuja kwa pamoja,” alisema.
Mhe. Kubecha alimaliza kwa kusema kuwa mchezo wa ngumi ni zaidi ya vita; ni mchezo wa kirafiki unaojenga upendo, mshikamano, na utayari wa vijana kutumikia taifa lao. Alisema kuwa, mbali na kuonyesha vipaji, mchezo wa ngumi pia unatoa fursa kwa vijana kusafiri kwenda mataifa mengine na kuitangaza Tanzania kimataifa.