Viongozi wa Geita Jogging leo wamepokea mwaliko wa heshima kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mheshimiwa Hashimu Komba, aliyealikwa ofisini kwake kwa lengo la kutoa shukrani za dhati na kuonesha kutambua mchango wa kikundi hicho.
Katika kikao hicho, Mheshimiwa Komba amewapongeza kwa mafanikio makubwa katika kushirikiana kufanikisha shughuli mbalimbali mwaka 2024, hususan zile zinazohamasisha mazoezi na afya bora, kama vile Geita Fitness Day. Tukio hilo limekuwa alama muhimu ya kuimarisha uelewa wa umuhimu wa mazoezi miongoni mwa wakazi wa Geita.
Mheshimiwa Komba amewahimiza kuendeleza juhudi hizo kwa ari zaidi mwaka 2025. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa Geita Fitness Day kwa kushirikisha wilaya za jirani kama Chato, Mbogwe na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro.
Kwa kuonesha dhamira yake ya kushirikiana na Geita Jogging, Mkuu wa Wilaya amethibitisha mchango wake wa shilingi 200,000 kwa ajili ya kufanikisha tukio la Geita Jogging Get Together, litakalofanyika tarehe 31 Desemba 2024. Aliongeza pia kuwa atashiriki kikamilifu katika tukio hilo.
Kwa upande wao, viongozi wa Geita Jogging wakiongozwa na Mwenyekiti, Vallence Ibrahim, pamoja na Makamu Mwenyekiti, Rosemary Steven, wamemshukuru Mheshimiwa Komba kwa jitihada zake za kuhamasisha mazoezi na afya bora miongoni mwa wananchi wa Geita.
Vallence Ibrahim ametoa wito kwa wananchi wote wa Geita na maeneo jirani kuendelea kushiriki kikamilifu katika mazoezi na kampeni mbalimbali za afya. Alisisitiza kuwa mazoezi ni msingi wa jamii yenye afya bora.
MWISHO