Na Mwandishi Wetu, Kalambo.
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo iliyopo Mkoani Rukwa, Mhe Tano Mwera ameshiriki zoezi la Sensa ya Watu na Makazi huku akitaka Wananchi kuendelea kujitokeza kuhesabiwa na kutoa taarifa sahihi kwa Makarani wa zoezi hilo lililoanza nchini kote Agosti 23, mwaka huu ambalo litaendelea kwa muda wa siku Saba.
“Nitumie nafasi hii kuwataka Watanzania na Wakazi wa Kalambo tuendelee kutoa ushirikiano kwa Makarani wa Sensa wanaopita kwenye Kaya zetu kutoa taarifa sahihi,” Alisema Mhe. Tano Mwera.
Pia ametoa wito kwa watumishi kuwa mstari wa mbele kuhesabiwa ikiwemo pia kuacha taarifa majumbani pindi wawapo kwenye majukumu yao ilikurahisisha zoezi hilo.
Wilaya ya Kalambo yenye jumla ya Tarafa 5, Kata 23, Vijiji 111 na Vitongoji 422, ni miongoni mwa Wilaya za pembezoni, huku ikiwa inapakana na Nchi jirani ya Zambia.
Mwisho.