Home Kitaifa CHUO CHA VIWANDA VYA MISITU FITI CHAAZISHA KOZI YA BIASHARA YA HEWA...

CHUO CHA VIWANDA VYA MISITU FITI CHAAZISHA KOZI YA BIASHARA YA HEWA KABONI*

CHUO cha Viwanda vya Misitu kimeanzisha kozi fupi ya biashara ya hewa kaboni ambayo imelenga kuifanya nchi kunufaika na zao hilo jipya la misitu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI), Dkt. Zakaria Lupala amesema asilimia 55 ya ardhi ya Tanzania ni hifadhi za misitu hivyo kuwa na fursa kubwa ya biashara ya hewa kaboni kwenye soko la kimataifa, lakini jamii haina ujuzi wa kunufaika na fursa ya biashara hiyo yenye mtazamo wa kuhifadhi mazingira.

Amesema pamoja na nchi kuwa na utajiri wa misitu, bado fursa ya biashara ya hewa ukaa haijatumika ipasavyo hatua ambayo imefanya Chuo hicho kuanzisha kozi fupi katika sekta hiyo.

“Chuo kimeamua kuongeza kozi ya zao lingine la mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu ambayo ni biashara ya hewa kaboni kwani pamoja na utajiri wa misitu lakini watanzania hawana ujuzi”

“Hapa nchini tuna kiwango kikubwa cha hewa kaboni, na tuchopungukiwa ni ujuzi kuhusu biashara hiyo na ndio maana tukaanzisha kozi fupi ya biashara ya hewa kaboni. Tunataka kampuni ambazo zitakuwa na ujuzi wa kutengeneza wadadisi kwenye biashara ya hewa kaboni.”

Amesema chuo hicho kinawataalamu bobezi katika fani hiyo ambao watasaidia watanzania kutengeneza kampuni za uwakala (carbon blocker), uandishi wa mawazo ya biashara ya hewa kaboni, upimaji na namna ya kufanya majadiliano ya biashara katika soko la kimataifa.

“Ndani ya wanyamapori kwenye hifadhi zetu, pia tunaweza kufanya biashara huku tukiwa tunatunza hifadhi zetu, nje ya wanyamapori tutapata motisha ya hifadhi.”

Naye Afisa Misitu Mkuu kutoka Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Emmanuel Msoffe ametoa rai kwa watanzania kutumia fursa ya Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi kuwapeleka vijana wao kupata mafunzo ili waweze kupata ajira na kipato katika kuendeleza maisha yao ya kila siku.

“Tumefika chuoni hapa na tumeona fursa mbalimbali ambazo kama zikitumiwa vizuri zinaweza kusaidia kuleta ajira, kazi na kipato na fedha za kigeni. Tumeona vijana na ubunifu wao na teknolojia mbalimbali ambazo wanazitumia katika kuhakikisha kwamba wanajipatia ajira na kipato.”

Msoffe amesema Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 na Mkakati wa Utekelezaji wa 2021 hadi 2031 unaelekeza uhifadhi misitu endelevu ili ufaidishe vizazi vijavyo.

Amesema kutekeleza hilo, Wizara kupitia idara imekuwa ikitoa elimu kwa umma ili umma uweze kuelewa faida na fursa zilizopo katika uhifadhi na misitu na nyuki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!