Katika kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza tarehe 16/06/2022 hadi 23/06/2022, Chuo cha Maji kimeamua kurudisha huduma kwa jamii kwa kufanya zoezi la upimaji wa sampuli za maji ya visima vinavyotumika kwa matumizi ya nyumbani bure kwa wakazi wa Dar es Salaam mia moja (100).
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar Es Salaam Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Adam Karia amesema kila sampuli moja inagharimu kiasi cha Tshs. 190,000/= ikijumuisha upimaji wa vigezo vyote ambavyo vimeelekezwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) .
Aidha Dkt. Karia amesema Kutokana na umuhimu wa kila mwananchi kuwa na haki ya kutumia maji safi na salama, wao kama taasisi yenye dhamana ya kutoa huduma na ushauri wa kitaalam katika Sekta ya Maji Nchini, kupitia Maabara yao ya Ubora wa Maji wanatoa nafasi kwa wakazi wa Dar es Salaam mia moja (100) kupimiwa ubora wa maji ya visima bure ili kujua hali ya maji hayo yanayotumika kwa matumizi ya nyumbani kama yamekidhi matakwa ya kiafya na kupatiwa ushauri wa kitaalam bila gharama yeyote.
“Zoezi la kupokea taarifa kwa wale watakaopenda kushiriki katika huduma hii limeanza tarehe 16/06/2022 mpaka pale idadi ya sampuli 100 zitakapokamilika, ambapo mshiriki unatakiwa kupiga simu kwenye namba 0718968582 au 0621879079 na kutoa taarifa zako sahihi ikiwemo jinsi ya wataalam wetu kukufikia na kuchukua sampuli ya maji kwa ajili ya upimaji” amesema Dkt. Karia
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Chuo cha Maji amesema mara baada ya kazi za upimaji zitakapokamilika. Majibu yatatolewa baada ya wiki mbili na yataambatana na semina ya kuelekeza wananchi jinsi ya kutumia maji kwa usahihi, njia salama ya utunzaji na uondoshaji wa majitaka na taka ngumu.
Kwa niaba ya Chuo cha Maji Dkt. Karia ametoa shukrani za dhati Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Hamidu Aweso kwa kutekeleza ahadi yake aliyoitoa mapema mwaka huu ya kukarabati mabweni yote matano ya Chuo cha Maji, ambapo ujenzi huo unaendelea.
Kwa upande wa taaluma Dkt.Karia amesema jumla ya wanafunzi waliosajiliwa kwa mwaka wa masomo 2021/2022 ni 2193,kati yao wanawake ni 846 ambao ni asilimia 39.
Pia Chuo kimeongeza kozi mpya za mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya Shahada(Degree) na Stashada(Diploma) katika fani mbalimbali ikiwemo,
Bachelor Degree in Community Development for Water Supply and Sanitation,
Bachelor Degree in Hydrogeology and Drilling,
Bachelor Degree in Engineering Hydrology,
Bachelor Degree in Sanitation Engineering,
Ordinary Diploma in Sanitation Engineering,
Kwa upande wa miundombinu ya Chuo Dkt. Karia amesema bajeti ya mwaka 2022/23 imelenga kuboresha miundombinu ya Chuo na ujenzi wa Kampasi ya Singida, ambayo imeshaanza kufundisha kozi mbili ambazo ni Water and Sanitation Engineering na Water Laboratory Technology, ambapo dirisha la udahili kwa wanafunzi wa mwaka wa masomo 2022 /2023 limeshafunguliwa.