Na Shomari Binda-Tarime
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM ( UWT ) Taifa Merry Chatanda amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya madiwani wa viti maalum kugomea harambee ya jumuiya hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Taifa agosti 28 kwenye ukumbini wa CMG Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa Ellen Bugoye amesema ni aibu kitendo walichokifanya madiwani hao.
Amesema madiwani wote wanazo taarifa juu ya ujio wa Mwenyekiti wa UWT Taifa na harambee hiyo lakini kutokana na makundi yasiyo na faida wameshindwa kufika
Ellen amesema madiwani wote kutoka Serengeti wameshindwa kufika na anazo taarifa za kutokufika kwao n a kushindwa kutoa michango kwamba watapampa sifa Katibu wa UWT wa Wilaya.
Mwakilishi huyo wa Mwenyekiti wa UWT Taifa amesema madiwani kutoka Butiama nao wameshindwa kufika jambo ambalo linatia aibu.
” Katibu wa CCM mkoa huko hapa hii ni aibu hawa madiwani ambao hawajafika waandike barua za kujieleza wakuletee na utume nakala ngazi ya Taifa.
” Hatuwezi kukubaliana na hiki ambacho kimetokea na taarifa ntafikishia Mwenyekiti wanapokuwa wanataka nafasi wanakuwa wapole kwenye kusaidia jumuiya wanaleta makundi”,amesema.
Katibu wa UWT mkoa wa Mara Saidan Mwamba amesema wanakusudia kukusanya kiasi cha shilingi milioni 100 kwa kuanzia katika kusaidia vitega uchumi vya jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi ya UWT mkoa wa Mara Marian Sagini amesema lengo la kuandaa harambee hiyo ni kuondoa utegemezi kwa jumuiya hiyo na kuanzisha miradi ya kiuchumi.
Mariam amesema harambee hiyo sio mwisho bali kamati yake itaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kupata fedha za kuisaidia jumuiya.
Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Mara Nancy Msafiri amesema siasa bila uchumi haiwezi kwenda hivyo lazima jumuiya isonge mbele kwa kuwa na vitega uchumi
Amesema kila mmoja anapaswa kujitoa kuchangia jumuiya ili kazi zake ziweze kufanyika ikiwa ni pamoja na kufanya ziara za uimalishaji umoja huo.