Na Scolastica Msewa, Chalinze.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani limepitisha ujenzi wa hoteli ya hadhi ya nyota tano na kituo cha kuuza mafuta Petrol Stationi ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kuongeza vyanzo vya mapato vya halmashauri hiyo.
Akiwasilisha taarifa kwenye Baraza la Madiwani la robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 ya kuanzia mwezi julai hadi septemba Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Hassani Mwinyikondo alisema miradi hiyo itaongeza mapato katika halmashauri hiyo kwani dhamira ya serikali ni kuongeza vyanzo vya mapato ili kujitegemea.
“Tunashukuru tayari tumefanya mazungumzo na shirika la Nyumba NHC tumekubaliana maana tunataka tuwekeze mradi wa Hoteli yenye ukumbi wa Kisasa wao wamekubali kutujengea Hoteli ya hadhi ya nyota tano hapa kwetu Chalinze”
“Na hivyo sasa tumekuja kupitisha kwenye Baraza la Madiwani leo ili hatimaye ujenzi uanze naamini kwamba wakifanikiwa kujenga hiyo hoteli tutakuwa na kiwango kikubwa zaidi cha mapato”
“Kwanza uwezo wa kurejesha tunao tuwatoe hofu wale wajenzi kwani sisi halmashauri ya Chalinze kama tunakusanya shilingi bilioni 15 tutashindwaje kurejesha fedha kwaajili ya jengo hilo?” alihoji Mwinyikondo.
“Kwasababu tukirejesha na pato letu litakuwa kubwa sana kwani leo Chalinze hakuna Hoteli yenye hadhi nzuri ya mtu kuja kulala mfano waheshimiwa wabunge wala waheshimiwa mawaziri na tutapata pato kubwa” alisema.
Alisema Halmashauri ya Chalinze inalipa katika petrol station ya kawaida kwa robo mwaka zaidi ya milioni 90 hivyo wakiwa na petrol station yao zile fedha wanazolipa kwenye petrol station za wazabuni sasa mapato hayo yataingia moja kwa moja kwenye halmashauri ya Chalinze.
“Mimi nina imani ndani ya mwaka mmoja au miaka miwili gharama ya ujenzi wa petrol station itakuwa imekamilika na baada ya hapo litakuwa ni pato kuanzia kwenye vyanzo vya mapato vya halmashauri” alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze Radhamani Possi amesema fursa nyingi zinafunguka Chalinze kwasababu ya ukaribu wake na bandari kavu ya Kwala ambapo wawekezaji wengi wanakwenda Chalinze kuwekeza.
Alisema lakini miundombinu ya kuwawezsha wawekezaji hazikuwa za kutosha hivyo walitafuta wabia ambao wataweza kuendesha nao hiyo miradi.
“Tumepata Wabia ambao tunakwenda kutekeleza kwa kupata hoteli ya hadhi ya nyota tano yenye ukumbi wa kisasa ambayo itaweza kuendesha shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikutano ili kuongezea kipato Halmashauri” alisema.
“Hivyo tuliingiza kwenye baraza kupata ridhaa ndio tuanze mchakato sasa wa kufanya maandalizi ya jumla ya ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kujua gharama ya ujenzi wake itagharimu kiasi gani na kuangalia makubaliano mengine kisha tutarudi kwenye baraza kuomba kupitishiwa maamuzi hayo” alifafanua Possi.
“Lakini jingine tumezungumzia suala la kuanzisha petrol station ambayo itakuwa ni mali ya halmashauri hii itakuwa na maana mbili yaani kwa maana ya kipato kwa halmashauri na itaenda kutoa huduma kwa sisi badala ya kuwa tunakwenda kwenye petrol station basi tutaweza kuwa wenyewe gari zetu zitakuwa zinakwenda kupata mafuta na tukinunua kwa wingi hata ile gharama itapungua badala ya kununua kupitia wazabuni” alisema Possi.