Wafanyakazi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliopandisha Bendera yenye Picha ya Rais na ujumbe wa Kodi kwenye Kilele cha Mlima Kilimanjaro wamekabidhiwa vyeti vya kupanda Mlima Kilimanjaro na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Mwenda.
Akizungumza wakati wa kuwakabidhi vyeti hivyo Kamishna Mkuu Mwenda amesema wameiheshimisha TRA kwa kupeleka ujumbe wa Kodi Kileleni jambo ambalo litahamasisha watu wengine kupanda Mlima Kilimanjaro na kuendelea kulipa Kodi.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema kutokana na sekta ya Utalii kuwa ni wachangiaji wakubwa wa Kodi kwa TRA ipo haja ya mameneja wote kupanda Mlima msimu ujao.
“Mameneja jiandaeni kupanda Mlima Kilimanjaro ili tulete Hamasa zaidi ya masuala ya Utalii na kuchochea kulipa Kodi” CG Mwenda.
Vyeti hivyo vilikabidhiwa katika ofisi za Kampuni ya Utalii ya ZARA ambako Kamishna Mkuu Mwenda ameahidi kuendelea kushirikiana na Walipakodi wa sekta ya Utalii ili waendelee kulipa Kodi.
Amesema TRA ni rafiki wa Mlipakodi hivyo wakiwa na changamoto wanapaswa kuzungumza ili wazitatue kwa pamoja.
Kwa upande wa Kampuni ya ZARA Afisa Rasilimali watu wa Kampuni hiyo Benard Sahiru amemuomba Kamishna Mkuu wa TRA awasaidie kuzungumza na mamlaka zinazotoka vibali vya kurusha Ndege ndogo Drone kwaajili ya kupigia picha wapunguze urasimu.
Amesema kumekuwa na ucheleweshaji wa kutolewa kwa vibali vya kurusha Drone Hali inayopoteza Mapato kwa baadhi ya watalii kukosa huduma hiyo.
Benard Sahiru ameomba kama upo uwezekano vibali hivyo viombwe na kutolewa mtandaoni jambo ambalo Kamishna Mkuu wa TRA ameahidi kulifanyia kazi kwa kufuatilia kwenye Mamlaka zinazohusika.