Home Kitaifa CG MWENDA AWAONYA WANAOGHUSHI RISITI ZA EFD

CG MWENDA AWAONYA WANAOGHUSHI RISITI ZA EFD

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Bw. Yusuph Mwenda, ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wachache wanaojihusisha na ukwepaji kodi kupitia mauzo hewa na risiti bandia.

Akizungumza Ijumaa, Desemba 20, 2024, wakati wa ziara yake ya kuwashukuru walipakodi katika Soko la Kariakoo, Mwenda amesema kuwa tabia hiyo ni kosa linalohujumu uchumi wa nchi.

“Kuna wachache wanakwepa kodi kwa kufanya mauzo hewa, wanaonesha wamemuuzia mtu bidhaa za thamani kubwa wakati hawajafanya mauzo hayo, risiti hizi bandia zinatumika kupunguza malipo ya kodi yanayostahili kulipwa” CG Mwenda.

“Tunawajua wanaofanya hivyo, na vyombo vyetu vinaendelea kufuatilia, Wito wangu ni kwamba waache mara moja, vinginevyo watakamatwa na watahitajika kulipa kodi pamoja na riba na penati,” amesema Mwenda.

Amewahimiza wafanyabiashara wa Kariakoo kuhakikisha wanatii sheria za kodi na kuepuka kujihusisha na ununuzi wa risiti hizo bandia, akisisitiza kuwa TRA imeimarisha mifumo yake ya ufuatiliaji ili kudhibiti ukwepaji kodi kwa ufanisi.

Nao wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wamepongeza juhudi za TRA katika kuwaelimisha na kuwahamasisha kulipa kodi kwa njia rahisi na salama. Bashiir Mohammed, mmoja wa wafanyabiashara, amesema:

“Sasa hivi kuna uelewa wa kutosha, na kila mfanyabiashara amewezeshwa kufahamu namna ya kulipa kodi kupitia mifumo ya TRA. Ninawashauri wenzangu tuwe waaminifu na tulipe kodi bila kulazimishwa.”

Naye Peter Joseph amewasihi wafanyabiashara wenyewe kuwa mstari wa mbele kulipa kodi bila kusubiri kufuatiliwa isipokuwa wanapofanya biashara waatakiwa kwenda TRA kwa makadirio na kulipa kodi yao.

Ziara ya Kamishna Mkuu wa TRA katika Soko la Kariakoo imelenga kuimarisha mahusiano kati ya mamlaka hiyo na wafanyabiashara, sambamba na kusisitiza umuhimu wa kodi katika maendeleo ya nchi.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!