Na Boniface Gideon,TANGA
Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimewapiga jeki Vijana wanaojihusisha na Biashara ya kuuza nyama na Mafundi Magari walipo katika soko kuu la Jiji la Tanga ( Mgandini). Chama hicho kimetoa Fedha kwaajili ya kununua vitendea kazi ikiwemo Mitambo ya kuchunguza tatizo la gari, mtambo wa kujaza upepo na Vifaa vya Michezo.
Akizungumza jana kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya kukagua na kuzindua Matawi ya chama hicho, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajab Abdallarrham alisema chama hicho kitahakikisha kinaisimamia Serikali ili Vijana wapate Mikopo ya Halmashauri.
“Leo tumekuja hapa sokoni kuona changamoto mlizonazo Vijana, mmesema mnahitaji Mitambo ya kuchunguza tatizo la gari pamoja na mtambo wa kujaza upepo na vifaa vya michezo, basi chama kimewasikia na tunawakabidhi fedha Sh.4,500,000 ili mpate kununua vitendea kazi kama mliomba” Alibainisha Rajab
Aliwataka Vijana kuacha tabia ya kukaa vijiweni bila kazi kwa kisingizio cha ukosefu wa ajira,
“Vijana fanyeni kazi kwa bidii, acheni kukaa vijiweni na kuongea umbea asubuhi hadi jioni, fanyeni kazi, ukifanya kazi Mungu nae anakufungulia milango ya kipato na kuongeza maarifa zaidi, Chama kitaendelea kuisimamia Serikali hususani kwenye utoaji wa Mikopo ya Halmashauri kuanzia mwezi wa Saba” Alisema Rajab
Wakati huo huo Chama hicho kimeibomoa Ngome za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)Mkoa wa Tanga kwakuwachukua Vigogo watatu wa ngazi za juu katika chama hicho akiwemo Aliyekuwa Diwani wa Viti maalumu Wilaya ya Muheza Ashura Kachenje ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wanawake Wilaya ya Muheza (BAWACHA).
Wengine ni Aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Tanga ambaye aliratibu Maandamano ya Amani wiki iliyopita pamoja na Katibu wa BAWACHA Wilaya ya Tanga,
“Tumeamua kurudi CCM ili kuja kumuunga mkono Rais Samia, kwakuhakikisha anashinda kwakishindo ,na tutaanza na serikali za mitaa na mwakani tutashinda uchaguzi Mkuu kwakishindo” Alisema Ashura Kachenje Aliyekuwa Diwani wa Viti maalumu Wilaya ya Muheza
MWISHO