Na Magrethy Katengu
Dar es salaam
KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla amewashukuru wananchi kwa kukiamini chama hicho kushinda kwa kishindo nafasi za uongozi wa ngazi kuanzia Serikali za mitaa Ujumbe na wenyeviti wa vijiji kwani hiyo yote ni maandalizi waliyoyafanya pamoja na kuzitumia 4R za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kama nyenzo yake kuu.
Shukrani hizo amezitoa leo Novemba 29, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam.
Amebainisha kuwa, sababu zilizoipa ushindi CCM kuwa ni pamoja na wananchi kuridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020/2025, vyama vya upinzani kutojiandaa na uchaguzi huo ikiwa pamoja na migogoro iliyopo ndani ya vyama hivyo.
“Niseme sababu moja wapo ya CCM kushinda ni pamoja na wananchi kuridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020/2025, na vyama vya upinzani kutojiandaa na uchaguzi lakini pia nyingine ni migogoro iliyopo ndani ya vyama vyao nyie wenyewe mashahidi kwa yale yaliyokuwa yanaendelea kule Arusha chama kimoja kuwa na mgogoro wa ndani ya chama chao.
“Lakini CCM huwezi kusikia hayo yakitokea ni kwasababu kila siku chama kinatoa mafunzo kwa maafisa wake pamoja na viongozi wa chama na ninashukuru nikiwa kama mlezi wa Dar es Salaam kuona imechukua Mitaa 563 kasoro mmoja ambao umeenda ACT Wazalendo,” amesema Makalla.
Amesema, uchaguzi ulikuwa na hamasa kubwa katika chama na watanzania kwa ujumla, hususani kwenye kujiandikisha katika daftari, kampeni na kupiga kura.
Amefafanua kuwa, kufuatia matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yaliyotangazwa jana na Waziri, Ofisi ya Rais, Tawara za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohammed Mchengerwa na kukitaja chama hicho kupata ushindi wa Mitaa kwa asilimia 98.8, Vitongoji asilimia 98, Wajumbe wa Vijiji asilimia 99 na Wajumbe wa Mitaa asilimia 99, hiyo imeamsha hamasa kubwa kwa chama hicho kuendelea kuwatumikia wananchi kwa weledi.
“Jana tumeshuhudia Waziri Mchengerwa akitangaza matokeo ya uchaguzi na nyie ni mashahidi kwamba matokeo yaliyotangazwa yameipa ushindi CCM wa kishindo. Hii inamaanisha kuwa tulijiandaa vizuri na kufanya kampeni za kisayansi.
“Lakini wakati sisi tunakiboresha chama kwa kuzunguka Mikoa yote 20 na kusikiliza kero za wananchi, kuangalia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya 2020/2025 wenzetu wao hawakufanya hivyo walikuwa bize na maandamano na wengine kwa takribani ya miezi saba inasemekana hawakuonekana katika maeneo yao wameenda kipindi cha kampeni ndiyo utegemee chama hicho kishinde kweli?,” amehoji Makalla.
Hata hivyo, Makalla amewataka viongozi wote wa CCM waliochaguliwa kwenda kuwajibika kwa wananchi kwa kusoma taarifa za mapato na matumizi na kutoa huduma bora ili kubeba dhamana na imani waliyopewa .
“Kampeni zimeisha na hivi sasa sisi ni wamoja hivyo nitoe rai kwa viongozi wa Serikali na chama tawala kutoa ushirikiano kwa viongozi wa vyama vyote bila kubagua kwani viongozi wote waliochaguliwa wametokana na imani ya wananchi katika maeneo yao.
“Tufanye siasa kwa kushindana kwa hoja lakini inapofika suala la kuwatumikia wananchi tuache mambo mengine pembeni na tujenge nchi yetu,” amesema Makalla.