Home Kitaifa CCM YASEMA HAKUNA CHAWA WALA KUNGINI, MAFANIKIO YAPO KATIKA JUMUIYA

CCM YASEMA HAKUNA CHAWA WALA KUNGINI, MAFANIKIO YAPO KATIKA JUMUIYA

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) anayeshughulikia Oganaizesheni na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Issa Gavu, ametoa wito kwa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) kuongeza juhudi za kuandikisha wanachama wapya ili kufikia wanachama milioni tisa kutoka milioni 6.1 waliopo sasa.

Akizungumza Desemba 15, 2024, katika Mkutano wa Baraza la UWT uliofanyika mkoani Tanga, Gavu aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, alielezea kuridhishwa kwake na mafanikio ya UWT yaliyoelezwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Marry Chatanda, ikiwemo ongezeko kubwa la wanachama wapya.

Gavu alieleza: “Naamini hii ni chachu katika safari ya kutafuta ushindi wa chama chetu mwaka 2025. Nawapongeza kwa mafanikio makubwa tangu kuingia kwenu madarakani. Kwa kipindi cha miezi 12, mmeongeza wanachama milioni mbili, kutoka milioni 4.1 hadi milioni 6.1. Hongereni sana!

Alisisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi zaidi katika kuandikisha wanachama wapya, akibainisha kuwa idadi ya wanachama ni msingi wa ushindi wa chama katika chaguzi zijazo.

Kasi yenu ni nzuri, lakini tunahitaji kuifikisha jumuiya yetu katika wanachama milioni tisa ifikapo mwisho wa mwaka huu. Hii itachangia kufanikisha malengo ya CCM ya kuwa na wanachama milioni 12.”

Gavu alitoa mwongozo kwa watu binafsi au taasisi zinazotaka kushirikiana na CCM, “Wanaohitaji kushirikiana na chama chetu lazima wafuate miongozo na taratibu zinazotolewa. Hatutoruhusu mtu binafsi kujitangaza kuwa msemaji wa chama au Rais wetu. Mfumo wetu unaheshimu maamuzi ya vikao rasmi, ambavyo ni Mkutano Mkuu, Halmashauri Kuu, na Kamati Kuu.”

Alionya juu ya watu wanaojifanya wamepewa mamlaka maalum na viongozi wakubwa wa chama kwa lengo la kuwababaisha wanachama. “Chama chetu hakina chawa, kunguni wala mtu aliye juu ya mfumo. Uamuzi wa chama unafanyika kupitia vikao vyake halali.

Gavu alisisitiza kuwa UWT ni sehemu muhimu ya ushindi wa CCM, “Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tulisimama sisi wenyewe – wana CCM na jumuiya zetu. Mafanikio hayo ni kielelezo cha muundo thabiti wa chama chetu. Ushindi huo tutaupeleka kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.

Alitoa wito kwa wanachama waendelee kupigania chama na jumuiya zao kwa bidii huku wakizingatia taratibu na maadili ya CCM.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!