Home Kitaifa CCM TANGA YAKARIBISHA WAWEKEZAJI

CCM TANGA YAKARIBISHA WAWEKEZAJI

Na Paskal Mbunga, Tanga.

CHAMA cha Mapinduzi, Mkoa wa Tanga kimewakaribisha wawekezaji wanaotaka kuwekeza maeneo mbalimbali ya kibiashara yanayomilikiwa na Chama hicho mkoani hapa kwa lengo la kuongeza wigo wa mapato.

Akizungumza ofisini kwake na waandishi habari mwishoni mwa juma lililopita, Katibu wa CCM wa Mkoa huu, Mzee Suleimani Mzee alisema uamuzi huo unakwenda sambasamba na maagizo ya CCM-Taifa yaliyoko kwenye Ilani yake ya Uchaguzi.

Kauli hiyo ya Katibu wa Mkoa imekuja masaa machache tu baada ya kuhitimisha sherehe kubwa ya ufunguzi wa tawi la Benki ya NMB katika moja ya jengo la Ofisi yao ya Mkoa lililokodishwa kwa NMB.

Mzee Suleimani alisema Chama cha Mapinduzi kimedhamiria kushirikiana na yeyote aliye tayari kuwekeza katika maeneo wanayomiliki, aidha kwa kukodi au kushirikiana kwa ubia (joint venture).

Alisisitiza kuwa Ofisi ya CCM ya Mkoa tayari imeanza kuonyesha njia ya namna uwekezaji unavyoweza kuleta tija ya moja kwa moja kwa pande zote mbili – mwekezaji na mwenye raslimali.

“Ufunguzi huu wa tawi la NMB hapa katika moja ya majengo yetu ni uthibitisho tosha namna tulivyodhamiria kushirikiana na wawekezaji”. Alisema na kuongeza ” hapa tunashuhudia CCM (M) watapata chao, NMB nao watavuna chao, lakini pia wananchi watafaidika kwa kusogezewa huduma karibu”.

Katibu wa Mkoa pia alifahamisha kwamba CCM Mkoa imekarabati uwanja wa mpira wa Mkwakwani kwa gharama ya zaidi ya milioni 65 ambapo baada ya kukamilika matengenezo , uwanja huo sasa uko tayari kwa shughuli mbalimbali za uwekezaji kwani utatumika masaa 24= mchana na usiku.

Aliyataja maeneo ambayo tayari yametengwa kwa uwekezaji ni pamoja na maeneo ya ufukweni mwa bahari (beaches) zikihusishwa wilaya za Mkinga, Tanga, Muheza na Pangani. Alisisitiza maeneo hayo ni mazuri kwa kujengwa mahoteli na sehemu za burudani.

Aidha kwa jiji la Tanga, Katibu wa Mkoa alibainisha kwamba yapo maeneo mengi kwa uwekezaji kuliko wilaya nyingine yeyote hapa mkoani. Aliyataja maeneo ya Raskazone ambapo mwekezaji/wawekezaji wanaweza kujenga hoteli za kitalii za Nyota Tano.

Alilitaja eneo jingine kubwa na maarufu kwa jina la ‘Kijiji cha Miaka 20 ya TANU’ akisema kuwa mwekezaji atakayepatikana, atatakiwa ajenge nyumba za kisasa za ghorofa (mall) zikiwa na maduka ili kuhudumia wakazi wa jiji hili linalozidi kupanuka kwa idadi ya watu.

Kuhusu utaratibu utakaotumika katika uwanja wa Saba-Saba ulioko Gofu Juu, Mzee Suleimani alisema uko wazi kwa wawekezaji wakubwa na wadogo huku akiwahakikishia wapangaji wa zamani kwenye eneo hilo kwamba hawatafukuzwa isipokuwa watatafutiwa maeneo mengine ya kuendelea na shguhuli zao.

Alisema uwekezaji katika wilaya za Pangani na Mkinga utahusu zaidi maeneo ya pwani ambapo wawekezaji wanakaribishwa kujenga hoteli za kisasa pamoja na maduka. Hata hivyo, alieleza kwamba jingo la sasa la CCM (W) ya Pangani litabomolewa na kungwa jingine kubwa la ghorofa nne ambapo ghorofa moja litatengwa kwa matumizi ya Ofisi za CCM na Jumuiya zake wakati ghorofa zilizobakia zitachukuliwa a mwekezaji kawa mkataba.

Kuhusu wilaya za Muheza na Korogwe, Katibu wa Mkoa alieleza kwamba mabadiliko makubwa yatakayofanyika ni kwenye ujenzi wa ofisi ambapo kutajengwa ofisi za ghorofa na wawekezaji watapewa baadhi ya ghorofa kwa kupangishwa. Wilaya nyingine za Lushoto, Handeni na Kilindi zitaingizwa katika mpango wa baadaye wa uwekezaji

(mwisho)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!