Home Kitaifa CCM MKOA WA MARA YAMKABIDHI MBUNGE PROF. MUHONGO TUZO YA UCHAPAKAZI

CCM MKOA WA MARA YAMKABIDHI MBUNGE PROF. MUHONGO TUZO YA UCHAPAKAZI

Na Shomari Binda-Musoma

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara kimemkabidhi mbunge wa jimbo la Musoma vijijini, Prof.Sospeter Muhongo tuzo ya uchapakazi.

Tuzo hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa chama hicho wa mkoa huo Patrick Chandi kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM.

Akikabidhi tuzo kwa mbunge huyo Chandi amesema Muhongo amekuwa mstari wa mbele kuchapa kazi jimboni ambazo zinaonekana hivyo kustahili kupongezwa.

Amesema tuzo hiyo ina thamani na itaongeza uchapakazi kwa mbunge huyo na kutia hamasa kwa viongozi wengine wakiwemo wabunge kuendelea kuchapa kazi.

Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Mara amesema Muhongo amekuwa akionekana uchapakazi wake kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za elimu pamoja na afya.

Amesema katika elimu Muhongo amekuwa akionekana kuchangia mifuko ya saruji na vifaa vingine vya ujenzi ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.

“Tunatambua mchango wa mheshimiwa Muhongo kwenye jimbo la Musoma vijijini katika shughuli za maendeleo na leo tunamkabidhi tuzo ya uchapakazi”

“Tuzo hii itakuwa chachu ya kuendelea kufanya kazi kwa kasi ya kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo na kuongeza hamasa kwa viongozi wengine” amesema Mwenyekiti huyo.

Akipokea tuzo hiyo,mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof.Sospeter Muhongo amekishukuru Chama cha Mapinduzi kwa kutambua mchango wake na kumtunuku tuzo hiyo.

Amesema tuzo hiyo itamfanya kuendelea kuchapa kazi kwa kuwatumikia wananchi wa jimbo la Musoma vijijini na Chama cha Mapinduzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!