Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Khadija Nasri Ally amewataka maofisa ugani walioajiriwa na bodi ya korosho Tanzania CBT kutoa elimu kwa Wakulima wa zao la korosho wa mkoa wa Pwani ili wanufaike zaidi na zao hilo kiuchumi.
Amesema hayo mjini Mkuranga wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano ya kujengewa uwezo maofisa ugani 29 walioajiriwa na bodi ya korosho Tanzania -CBT- walio katika mpango wa kukuza ujuzi kwenye programu ya Jenga kesho illiyobora .
Amesema Wakulima wengi hulima zao la korosho kwa uzoefu wa kimila na kizamani ambao hauna tija kwao hivyo maofisa ugani hao wakatoe elimu kwa Wakulima jinsi ya kuendeleza kilimo chao hata kiwaletee faida.
Khadija amesema Wakulima wafundishwe namna ya kutunza mikorosho yao kwa kujua namna ya upuliziaji wa dawa, muda sahihi wa kupulizia dawa , umuhimu wa kupalilia mashamba yao ya korosho ili wapate mavuno mengi katika kilimo chao hicho cha korosho na wapate faida.
Aliongeza kuwa iwapo mkulima akuhamasishwa kulima na akahamasika akalima inabidi apate faida na sio hasara kwani akipata hasara anakata tamaa anaweza asiendelee na kilimo hicho.
Alisema hakuna serikali duniani inayoweza kutoa ajira kwa Vijana wote katika taifa lao na ndio maana serikali ya Tanzania inaandaa programu mbalimbali ambazo zitasaidia Vijana na wananchi kwa ujumla’ kujiajili wanufaike kwa Fursa za programu hizo na wapate faida.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ya Mkuranga amezitaja baadhi ya kazi wanazotakiwa kwenda kuzifanya kwa Wakulima wa korosho mkoani Pwani kuwa ni pamoja na kuhuisha kanzidata ya Wakulima wa korosho, kusimama usambazaji wa pembejeo kwa Wakulima, kutoa elimu ya matumizi sahihi na salama ya viuatilifu kwa Wakulima na kufufua mashamba pori ya zao hilo la korosho mkoani humo.
“Majukumu mengine ni Kusimamia ubora na mfumo wa uuzaji wa korosho, kuwatembelea Wakulima mashambani na kuwadhauri kuhusiana ba mbinu bora za kilimo cha korosho ikiwa ni pamoja kukusanya takwimu za korosho zinazobaki majumbani kwa ajili ya kujumuishwa kwenye uzalishaji wa kitaifa” alisema Khadija.
“Nendeni mkawasaidie Wakulima kwani zao la korosho ni zao la kiuchumi na ni zao la kimkakati nchini hivyo ni lazima tuliendeshe kisomi kwa utaalamu stahiki Wakulima wanufaike na taifa nalo linufaike”. Alisema Khadija.
Naye Mwakirishi wa Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania CBT ambaye ni Kaimu Meneja wa Bodi ya korosho CBT tawi la Dar es salaam Domina Mkangara amesema Mafunzo hayo ya maofisa ugani 29 yatanufaisha wilaya sita za mkoa wa Pwani ambazo zinazalisha kwa wingi zao hilo la korosho.
Amesema huduma hiyo itaendelea kuongezwa kulingana na mahitaji ambapo lengo likiwa ni kusogeza huduma ya maofisa ugani karibu na Wakulima hasa kumekuwa na Changamoto ya huduma ya maofisa ugani hususani kwa kilimo cha korosho na nyororo wa kuongeza thamani ya zao hilo.
Domina amesema Mafunzo hayo umeandaliwa na serikali kupitia wizara ya kilimo ambayo ilitoa maelekezo kwa bodi ya korosho iandae mafunzo hayo ili kuwa na kundi kubwa la wataalamu wa kusimamia kilimo cha zao hilo kuanzia kwa mkulima hadi kufikisha kwenye vyama vya msingi.
Akizungumza kwaniaba ya Waziri wa Ujenzi Abdalah Ulega Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Mkuranga SheIn Kilindo amesema Mafunzo hayo yatakuwa msaada kwa Wakulima wa korosho wilayani humo hususani kwa kundi la vijana ambalo limekuwa likiendesha kilimo cha korosho kienyeji bila utaalamu wowote hivyo Wakulima hawanufaiki kama inavyotakiwa.
Amesema zao la korosho ni tegemeo kwa Vijana Wakulima wa Wilaya hiyo ya Mkuranga hivyo kundi hilo la maofisa ugani kupata mafunzo hayo itasaidia kuongeza tija kwa Wakulima na Vijana wa zao hilo kwa ujumla.
++++