Na Theophilida Felician, Kagera
Mbunge wa jimbo la Bukoba mjini na Naibu wa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe Stephen Byabato aunga juhudi za vijana na akina mama wa kata ya Rwamishenye wanaojishughulisha na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kwakuwapatia mikopo yakuwaongezea nguvu ili kuongeza kiwango cha ufugaji.
Mhe. Byabato ameitoa mikopo hiyo kwa makundi hayo ya vijana wa chama cha mapinduzi na akina mama mara baada ya kuikagua miradi hiyo nakujionea hali halisi ya ufugaji wa samaki kwa vikundi hivyo.
Akiwa kwenye mkutano wahadhara mbunge Byabato amesema kuwa amekuwa akiunga mkono vikundi tofauti tofauti vinavyojimudu kuendesha shughuli mbalimbali za kusaidia kujiingizia kipato na jamii kwa ujumla kupitia mikopo ya KOPA KWA MBUNGE LIPA KWA MWENZAKO.
Vikundi hivyo amevikabidhi Sh. Milioni moja moja kwa kila kikundi pesa ambayo wataitumia muda kadhaa bila ya riba na badaye kukopeshwa kwa vikundi vingine kwa malengo ya kuwafikia wananchi wengi.
“Juzi wakati nafanya mkutano pale Kashai nilipata nafasi yakutoa mikopo kwa vikundi mbalimbali jumla ya mikopo yenye thamani ya Sh Milioni 16 nilitoa pale Kashai, pesa hizi siyo za Serikali siyo za Manispaa pesa hizi ni zangu binafsi nipesa yangu kutoka mfukoni nimejibanabana hapa na pale nimeleta nyumbani nanyie wenzangu mpate kidogo kidogo” amesema Mhe Byabato mbele ya wananchi.
Amefafanua kuwa anapendezwa na watu wanaojihimu katika shughuli mbalimbali zikiwemo za ujasilimali hivyo ameahidi kuendelea kuwa nao bega kwa bega kwa kila namna.
Mbali na hayo Mbunge huyo ameweza kutatua kero kadhaa za wananchi ikiwemo ya kulipa madai ya akina mama wawili ambao mmoja ni mjasiliamali wa kuchuuza nguo kando kando ya barabara kuu yakuelekea Uganda katika eneo la senta ya Rwamishe Sharfa Leonard aliyekuwa akidai Sh 162,000 kwa Askari mmoja wa Jeshi la Polisi aliyemdhurumu baada yakuchukuwa nguo zake kwa mkopo katika biashara hiyo tangu mwezi Juni mwaka huu 2023 pamoja na 187,300 za madai ya mama Mwatatu Katakweba ambaye alikuwa akiidai ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba ya Ankara ya maji yaliyochotwa kwake wakati wa ujenzi wa ofisi ya kata ya Rwamishenye kwa muda wa miaka mitatu iliyopita.
Mbunge huyo amesema kuwa ameguswa na kulipa madai hayo ili kuwaondolea kero wananchi hao ambao wamehangaika muda mrefu bila ya mafanikio ya malipo yao huku akisisitiza kudai pesa hiyo mwenyewe kwa wahusika.
Aidha ameelezea shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo zilizotekelezwa kata ya Rwamishenye ikiwemo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 40, barabara za mitaa, afya, taa za barabarani na mingine mingi ambapo amewahakikishia wananchi kuwa Serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassani inaendelea na kazi yakuleta fedha za ujenzi wa miradi katani humo na Jimbo zima la Bukoba mjini kwa ujumla.
Hata hivyo amelipongeza Jeshi la polisi chini ya Mkuu wa polisi wilaya ya Bukoba Bashir Abdul kwakazi kubwa ya kutatua kero ya kamata kamata holera ya maafisa usafirishaji (boda boda) iliyokuwa changamoto kubwa mjini Bukoba.
Mwisho amewashukuru wananchi wa Jimbo la Bukoba kwa namna wanavyoendelea kumpa ushirikiano kwa kila jambo katika kuleta amaendeleo Bukoba hivyo amewahidi kwamba ifika mwaka 2025 panapo majaaliwa ya mwenyezi Mungu atagombea ili kukitetea kiti chake kwa mara nyingine tena.
Kwa upande wao wananchi wameshukuru ujio wa mbunge huyo katika eneo la kata yao Rwamishenye na kuzitatua kero zao pamoja na kuwaeleza mazuri yaliyofanyika nayanayoendelea kufanyika katika maeneo yao ambapo wameweka wazi kuendelea kumpa ushirikiano wa hali na mali ili kufanikiwa adhima ya kuijenga Bukoba zaidi kimaendeleo.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kichama akiwemo Katibu wa CCM Bukoba mjini Danieli Muhina ambaye amewaeleza wananchi kwamba chama hicho kimeendelea kuisimamia vyema Serikali jambo ambalo limeiwezesha kufanya mambo mengi ya kimaendeleo hususani Bukoba na kwingineko nchini.
Muhina ameongeza kuwa chama hicho kwa upande wa Bukoba kiko imara kuliko watu wanavyodhani “yapo mambo yamefanyika hapa siku mbili tatu zilizopita wenye kuongea wameongea nawengine wakasema mbona chama kiko kimya? naomba niseme machache yafuatayo hivii, Mhe mbunge na wananchi mliopo hapa Jimbo letu la Bukoba liko salama, mbunge anafanya kazi yake vizuri madiwani wangu wote wanafanya kazi vizuri wenye nongwa zao tutakutana 2025 waacheni wafanye kazi zao vizuri, naomba ni mpongeze sana Mkuu wa Mkoa, Mkuu wetu wa Mkoa amefanya kazi nzuri ametuunganisha vizuri watu wa Bukoba anataka tuondoe matabaka anataka maendeleo tumuunge mkono” maneno yake akisisitiza Katibu Danieli Muhina