Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amemtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kama kiongozi mwenye hekima na busara ya kiwango cha juu katika kudumisha amani,umoja na mshikamano wa Watanzania.
Mhe. Makonda ametoa kauli hiyo leo Agosti 28, 2024 alipokuwa akiwakaribisha wakuu wa Taasisi na mashirika ya Umma, wanaokutana Jijini Arusha kwenye kikao kazi cha kuelekezana na kushirikishana mabadiliko ya kiutendaji kwenye taasisi na mashirika ya Umma nchini.
Mhe. Makonda ametoa kauli hiyo mara baada ya serikali ya Rais Samia kufanikiwa kuumaliza mgogoro uliokuwepo kwa wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, baada ya kutoa maelekezo kupitia kwa mawaziri walioambatana na Mhe. Makonda wiki iliyopita kwenda kuzungumza na wananchi wa Ngorongoro na kuondoa vikwazo na visababishi vya sintofahamu iliyokuwepo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Makonda amewaalika viongozi hao kuwekeza mkoani Arusha kutokana na mahitaji makubwa ya kumbi za mikutano, hoteli na hospitali za kisasa zitakazosisimua utalii wa matibabu kwenye mkoa huo kinara kwa utalii kwa upande wa Tanzania bara.