Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 06 Mei 2023 amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano kwaajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ukanda wa Maziwa Makuu (Peace Security and Cooperation Framework – PSC) uliofanyika Ikulu ya  Bujumbura nchini Burundi.
Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano kwaajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ukanda wa Maziwa Makuu ni Mfumo wa Uangalizi wa Ngazi ya Juu wa Kikanda kutoka nchi 13 zilizotia saini na Viongozi wa Mashirika manne ya Kimataifa yanayojulikana kama Wadhamini wa Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Ukanda wa Maziwa Makuu.
Mkutano huo unafanyika ikiwa Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano kwaajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ukanda wa Maziwa Makuu unatimiza Miaka 10 tangu uanzishwe mwaka 2013 jijini Addis Ababa nchini Ethiopia. Mpango huo ulianzishwa kwa lengo la kushughulikia changamoto za kiusalama na maendeleo nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Ukanda wa Maziwa Makuu ikiwa pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, nchi zilizotia saini na Mashirika manne ya Kimataifa yanayojulikana kama Wadhamini wa Mpango huo. Wadhamini hao ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za UKanda ya Maziwa Makuu (ICGLR), Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Hadi sasa Umoja wa Mataifa ambao ndiyo Mratibu wa Mpango huo kupitia Ofisi ya Mjumbe Maalum ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kama Mratibu Mweza kupitia Ofisi ya Mwakilishi wa Ngazi ya Juu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika imewezesha na kufanikisha jitihada mbalimbali kama vile Kuratibu Mikutano na Mazungumzo ya Amani,Kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zilizotia saini mpango huo pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kushirikiana kupitia majukwaa mbalimbali.