Home Kitaifa BUMBULI YAVUKA LENGO, YACHANJA WATOTO 33,159

BUMBULI YAVUKA LENGO, YACHANJA WATOTO 33,159

Na Yusuph Mussa, Bumbuli

HALMASHAURI ya Wilaya Bumbuli (Bumbuli DC) mkoani Tanga, imevuka lengo la uchanjaji chanjo ya ugonjwa wa polio kwa watoto chini ya miaka mitano baada ya kuchanja watoto 33,159 sawa na asilimia 110.7.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Septemba, 2022, Mratibu wa Huduma za Chanjo Halmashauri ya Wilaya Bumbuli Elizabeth Nyaki, alisema muitikio ulikuwa mkubwa katika tarafa zote tatu za halmashauri hiyo ambazo ni Bumbuli, Mgwashi na Soni.

“Hadi kumalizika kwa zoezi la chanjo ya polio kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano lililofanyika kwa siku nne (4) kuanzia Septemba Mosi hadi Septemba 4, 2022, tumeweza kuchanja watoto 33,159 sawa na asilimia 110.7. Na tumevuka lengo, kwani ilikuwa tuchanje watoto 29,936.

“Muitikio ulikuwa mkubwa, na wananchi walikuwa hawana wasiwasi na chanjo hiyo, kwani walipeleka watoto kwenye vituo wakisindikizwa na dada zao, na hata watoto waliotembelewa na wahudumu wa afya nyumbani, sokoni, stendi na kwenye magulio walichanja” alisema Nyaki.

Halmashauri ya Wilaya Bumbuli ilitarajia kuchanja chanjo ya ugonjwa wa polio watoto 29,936 wenye umri chini ya miaka mitano, ikiwa ni Awamu ya Pili ya chanjo hiyo baada ya Awamu ya Kwanza kuchanja chanjo hiyo kwa watoto 29,013.

Hayo yalisemwa Agosti 30, mwaka huu na Mratibu wa Huduma za Chanjo Msaidizi wa Halmashauri ya Bumbuli Kulwa Sadiki kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kwenye halmashauri hiyo.

Kulwa alisema Awamu ya Kwanza iliyofanyika Mei 18 hadi 21, mwaka huu, walitarajia kuchanja watoto wa umri huo 26,466, lakini baada ya zoezi kumalizika, walichanja watoto 29,013, hivyo kuongeza idadi ya watoto watakaopata chanjo kufikia 29,936 kwenye zoezi lililoanza Septemba Mosi, 2022 na litaendelea kwa siku nne (4) mfululizo.

“Zoezi la chanjo la ugonjwa wa polio kwa Awamu ya Kwanza, tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Makadirio yetu ilikuwa kuchanja watoto 26,466, lakini tuliweza kuchanja watoto 29,013. Hivyo malengo yetu sasa ni kuchanja watoto 29,936.

“Na tunatarajia kuwafikia watoto waliopo kwenye vijiji vyote 83 vya Halmashauri ya Bumbuli vilivyopo kwenye kata 18 katika tarafa tatu za Bumbuli, Mgwashi na Soni” alisema Sadiki.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!