Home Kitaifa BUMBULI YACHANJA WATOTO 10,377 SIKU YA KWANZA

BUMBULI YACHANJA WATOTO 10,377 SIKU YA KWANZA

Na Yusuph Mussa, Bumbuli

HALMASHAURI ya Wilaya Bumbuli mkoani Tanga, huenda ikavuka lengo la uchanjaji chanjo ya ugonjwa wa polio kwa watoto chini ya miaka mitano baada ya siku ya kwanza Septemba Mosi, 2022 kuchanja watoto 10,377.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi leo Septemba 2, 2022, Mratibu wa Huduma za Chanjo Halmashauri ya Wilaya Bumbuli Elizabeth Nyaki, alisema muitikio ni mkubwa katika tarafa zote tatu za halmashauri hiyo ambazo ni Bumbuli, Mgwashi na Soni.

“Hadi kufikia jana jioni Septemba Mosi,2022 tayari tumechanja watoto 10,377. Na tarafa zilizoongoza ni Bumbuli na Soni. Vituo vilivyoongoza kwa kufikia lengo na zaidi ni Bumbuli watoto 267 na Mavului watoto 242. Wengine wamefikia malengo, na ambao hawajafikia malengo wanaendelea kupambana kufikia lengo” alisema Nyaki.

Nyaki alisema hata siku ya pili ambayo ni Septemba 2, 2022, tayari muitikio ni mkubwa, na wananchi hawana wasiwasi na chanjo hiyo, kwani wanapeleka watoto kwenye vituo wakisindikizwa na dada zao, na hata watoto wanaotembelewa na wahudumu wa afya nyumbani, sokoni, stendi na kwenye magulio wanachanja.

Halmashauri ya Wilaya Bumbuli inatarajia kuchanja chanjo ya ugonjwa wa polio watoto 29,936 wenye umri chini ya miaka mitano, ikiwa ni Awamu ya Pili ya chanjo hiyo baada ya Awamu ya Kwanza kuchanja chanjo hiyo kwa watoto 29,013.

Hayo yalisemwa Agosti 30, 2022 na Mratibu wa Huduma za Chanjo Msaidizi wa Halmashauri ya Bumbuli Kulwa Sadiki kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kwenye halmashauri hiyo.

Kulwa alisema Awamu ya Kwanza iliyofanyika Mei 18 hadi 21, mwaka huu, walitarajia kuchanja watoto wa umri huo 26,466, lakini baada ya zoezi kumalizika, walichanja watoto 29,013, hivyo kuongeza idadi ya watoto watakaopata chanjo kufikia 29,936 kwenye zoezi lililoanza Septemba Mosi, 2022 na litaendelea kwa siku nne (4) mfululizo.

“Zoezi la chanjo la ugonjwa wa polio kwa Awamu ya Kwanza, tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Makadirio yetu ilikuwa kuchanja watoto 26,466, lakini tuliweza kuchanja watoto 29,013. Hivyo malengo yetu sasa ni kuchanja watoto 29,936.

“Na tunatarajia kuwafikia watoto waliopo kwenye vijiji vyote 83 vya Halmashauri ya Bumbuli vilivyopo kwenye kata 18 katika tarafa tatu za Bumbuli, Mgwashi na Soni” alisema Sadiki.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!