Home Kitaifa BRELA:WAKULIMA JITOKEZENI KUSAJILI BIASHARA ZENU

BRELA:WAKULIMA JITOKEZENI KUSAJILI BIASHARA ZENU

Na Monica Sibanda – Mzawa Online Dodoma

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wakulima kusajili nembo na alama za biashara zao ili kulinda biashara zao.

Akizungumza leo Agosti 4,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Ofisa Usajili kutoka BRELA Dodoma, Gabriel Girangay, amesema wakulima ni wadau muhimu kwa sababu wanapozalisha mazao wanayaongezea thamani hivyo kuhitaji kusajiliwa nembo au alama za biashara.

Wakulima ni wadau muhimu kwa sababu wanazalisha bidhaa mbalimbali na kuzipeleka sokoni ndiyo maana tunaendelea kutoa elimu watambue kwamba BRELA ni muhimu kwao katika kusimamia au kulinda bidhaa zao. Tutalinda vumbuzi zao katika masuala mbalimbali yanayohusiana na kilimo na teknolojia,” amesema Girangay.

Amesema wakala huo unafanya kazi ya kusajili kampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, kutoa leseni za biashara kundi A, leseni za viwanda, kusajili viwanda vidogo na kulinda vumbuzi za wataalam mbalimbali.

Tuko kwenye maonesho ya Nanenane kwa ajili ya kutoa elimu na huduma mbalimbali, ukifika katika banda letu utapata huduma za kusajiliwa jina la biashara na kila Mtanzania mwenye nia ya kuanzisha biashara afike kuna wataalam wa masuala ya Tehama, biashara, alama za biashara na huduma na shughuli zetu nyingi zinafanyika kidijitali.

Tunatoa leseni za biashara kundi A ambazo ni zile zenye sura ya kitaifa na kimataifa, utaelimishwa kwanza na kama unataka kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi au kutoa bidhaa kutoka nje na kuleta nchini utapata leseni BRELA,” amesema.

Kulingana na ofisa huyo, BRELA inatoa leseni za viwanda vikubwa na vya kati vyenye mtaji wa kuanzia Sh milioni 100 kwenda juu lakini Sh milioni 100 kwenda chini ni viwanda vidogo ambavyo pia wanavisajili.

Aidha amesema kama mtu anahitaji kupata taarifa yoyote kuhusu kampuni, majina ya biashara, leseni au wanaotaka kukopa na kuingia ubia wa kibiashara afike katika banda hilo au ofisi za wakala huo na atapatiwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!