Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), inashiriki katika Maonesho ya Sita (6) ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini ya mwaka 2023, kwa kutoa elimu na huduma mbalimbali za Sajili na utoaji wa Leseni.
Maonesho hayo yanafanyika katika viwanja vya Bombambili mjini Geita kuanzia tarehe 20-30 Septemba, 2023.
Banda la BRELA ni miongoni mwa mabanda ya Taasisi za Serikali ambazo zinashiriki katika Maonesho hayo ya Madini, ambapo inatumia jukwaa la maonesho hayo kuhamasisha wadau mbalimbali kurasimisha biashara zao pamoja na kutoa usaidizi kwa wadau wanaopata changamoto katika mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS).
Pamoja na kutoa elimu kwa Umma na usaidizi, BRELA pia inatoa huduma zote za Usajili na utoaji Leseni papo kwa papo.
Huduma hizo ni pamoja na usajili wa Majina ya Biashara, Kampuni, Alama za Biashara na Huduma, utoaji wa Leseni za biashara kundi “A”, Usajili wa Viwanda, utoaji wa Hataza, na huduma za kulipia ada za mwaka na uhuishaji wa taarifa za kampuni.
Maonesho hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 23 Septemba, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko na kufungwa rasmi tarehe 30 Septemba, 2023 na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.