Home Kitaifa BRELA yakutana na Taasisi za Udhibiti kuboresha mazingira ufanyaji biashara nchini

BRELA yakutana na Taasisi za Udhibiti kuboresha mazingira ufanyaji biashara nchini

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), inakutana na Taasisi za Udhibiti ili kujadili mikakati ya pamoja ya namna ya kutatua mikinzano inayojitokeza katika utendaji kazi wa kila siku, kutokana na Sheria, Kanuni na Taratibu zinazozimamia Taasisi hizo hapa nchini.

Akifungua Kikao Kazi Kati ya BRELA na Taasisi za Udhibiti, leo tarehe 13 Septemba, 2023, katika ukumbi wa Nashera Jijini Morogoro, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, ameeleza kuwa ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ni vyema kujadili kwa pamoja vikwazo vinavyosababishwa na usimamizi wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazotumika na kuangalia jinsi ya kuvikwamua, ili kukuza uchumi wa Tanzania.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuinua hali ya uchumi wa nchi, hivyo BRELA katika kuunga mkono jitihada hizo, inakutana nanyi ili kujadili mikinzano na muingiliano katika utoaji wa huduma na jinsi ya kuondokana na hali hiyo ili hatimaye kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa Tanzania hawakumbani na changamoto au uchelewaji wa kupata huduma hapa nchini”, amesema Bw. Nyaisa.

Ametoa mfano kuwa BRELA imekuwa ikikutana na changamoto katika utendaji na kusababisha usumbufu kwa wateja, pale ambapo Taasisi za Udhibiti zimekuwa zikitoa vibali vya biashara bila kujiridhisha endapo mfanyabiashara huyo amesajili Kampuni au Jina la Biashara ambapo athari kubwa anayoweza kuipata mfanyabiashara huyo endapo atapatiwa kibali wakati hajasajili Kampuni au Jina la Biashara ni kushindwa kusajili Jina la Biashara au Kampuni endapo jina husika litakuwa na ufanano na majina yaliyokwisha sajiliwa BRELA, hivyo mhusika kulazimika kubadilisha jina husika.

Ameendelea kusema kuwa athari kubwa anayoipata mfanyabiashara anaposhindwa kusajili jina linaloonekana kwenye Kibali alichokipata, huathiri biashara yake kama vile kukosa zabuni, mikopo au kuingia mikataba na Taasisi za Umma, kwa kuwa usajili wa Jina la Biashara au Kampuni ni hitaji la msingi katika mfumo wa sasa wa Ununuzi unaosimamiwa na PPRA uitwao NEST, ambao umeunganishwa na mfumo wa usajili kwa njia ya Mtandao( ORS) wa BRELA, ambapo mfanyabiashara hataweza kujisajili katika mfumo wa NEST kama hajasajili Kampuni au Jina la Biashara.

Naye, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bw. Lazaro Msasalaga, amesema kuwa kikao kazi hicho ni muhimu maana kinatekeleza malengo ya BluePrint kwa kuzingatia umuhimu wa wafanyabiashara kuwa na Leseni ya Biashara inayotolewa na BRELA na leseni zingine zinazotolewa na Taasisi za Udhibiti ikizingatiwa kuwa sheria hizo zilikuwepo kabla ya andiko hilo.

Washiriki wa Kikao Kazi hicho kutoka Taasisi za Udhibiti ambao ni Wanasheria pamoja na Maafisa wanaohusika na utoaji wa vibali mbalimbali, watapata fursa ya kujadiliana kwa siku tatu na kutoka na maazimio ambayo yatawasilishwa ngazi za juu ili kufanyiwa kazi.

BRELA, ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 na kuzinduliwa rasmi tarehe 3 Desemba, 1999 ikiwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Majukumu ya BRELA ni pamoja na Kusajili majina ya Biashara, Kampuni, Alama za Biashara na Huduma, Utoaji wa Hataza, Utoaji wa Leseni za Biashara Kundi “A” na Utoaji wa Leseni za Viwanda na Vyeti vya Usajili wa Viwanda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!