Home Kitaifa BRELA NA TAKUKURU WAFUNGUA MLANGO WA MASHIRIKIANO

BRELA NA TAKUKURU WAFUNGUA MLANGO WA MASHIRIKIANO

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA ) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), zimekusudia kuwa na mashirikiano ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Serikali.

Katika kufanikisha hilo, taasisi hizo zimekutana katika kikao kazi cha siku mbili tarehe 8 na 9 Julai, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano Nashera, mkoani Morogoro kujadili maeneo ya muhimu ya ushirikiano na changamoto zinazojitokeza wakati wa kutekeleza majukumu.

Bw. Godfrey Nyaisa, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, ameeleza kuwa Mkutano kati ya taasisi hizi utaleta maboresho makubwa ya kiutendaji kwa pande zote mbili.

“Tukiwa kama Wakala anayehusika katika kukuza uchumi kwa kurasimisha biashara, viwanda na uwekezaji nchini, tunajukumu la kuzingatia kuwa Sajili za kila aina zinafanyika kihalali na zinazingatia taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa sheria katika kuhalalisha biashara.

Ni matarajio yangu kwamba kikao hiki kitakwenda kuleta mabadiliko katika Taasisi zetu hususani kwenye changamoto mbalimbali tunazozipata ili kuleta ufumbuzi wa pamoja kwa manufaa ya Taasisi hizi mbili,” amesema Bw. Nyaisa.

Amebainisha kuwa kikao kazi hicho kitapitisha Rasimu ya Makubaliano (Memorandum of Understanding [MOU]) baina ya BRELA na TAKUKURU yenye dhamira ya kuleta umoja na mshikamano kwa Taasisi hizo katika kutimiza majukumu ya kila siku.

Akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni, Bw. Saimon Maembe, amesema kuwa kikao hicho ni muarobani wa changamoto sugu wanazokutana nazo katika utendaji kazi.

Bw. Maembe amefafanua kuwa taasisi hizi mbili zinafanya kazi kwa karibu sana hasa kwa kuwa taarifa zote kuhusu Makampuni zinapatikana BRELA na kuongeza kuwa, mara nyingi TAKUKURU imekuwa ikihitaji taarifa mbalimbali au ufafanuzi kuhusu taarifa za makampuni.

Kikao kazi hiki pamoja na mambo mengine, kinalenga kutengeneza mfumo mzuri wa kubadilishana taarifa, hasa kwa kuzingatia kuwa BRELA imeboresha upatikanaji wa taarifa kwa kuwa huduma zake zote zinapatikana kwa njia ya mtandao.

Kikao hicho kimehudhuriwa na washiriki zaidi ya 30 ambao ni Makamanda wa Kanda zote za Dar es Salaam, Wakurugezi wa Uchunguzi na Maafisa
uchunguzi kutoka Dar es Salaam na Makao Makuu Dodoma pamoja na Maafisa Usajili kutoka BRELA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!