Home Kitaifa BRELA KUCHOCHEA UJIO WA WAWEKEZAJI NCHINI

BRELA KUCHOCHEA UJIO WA WAWEKEZAJI NCHINI

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), itaendelea kutoa elimu kuhusu dhana ya Wamiliki Manufaa wa kampuni ili wawekezaji waendelee kuiamini nchi na kuendelea kuwekeza.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 15 Machi, 2023 na Kaimu Mkurugenzi wa Makapuni na Majina ya Biashara kutoka BRELA, Bw. Mainrad Rweyemamu wakati akifungua mafunzo siku mbili kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa, kuhusu dhana ya Wamiliki Manufaa kwa vyombo vya uchunguzi, yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Amboseli, Jijini Mwanza.

Bw. Rweyemamu amesema elimu hiyo kwa vyombo vya uchunguzi itawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kusimamia sheria na kuweka mazingira mazuri ya biashara kwa wawekezaji.

Hii itaisaidia nchi yetu kupata wawekezaji sahihi na wenye nia njema sio kufadhili ugaidi au mambo mengine yasiyofaa”, amesema Bw. Rweyemamu.

Ameongeza kuwa katika kukabiliana na wimbi la utakatishaji fedha, ukwepaji kodi pamoja na ufadhili wa ugaidi unaofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu katika kampuni, Wakala inavishirikisha kwa pamoja vyombo vya Uchunguzi vilivyoidhinishwa kisheria katika upatikanaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa wa kampuni kwa kuwapatia elimu ya kudhibiti vitendo hivyo.

Leo katika Ukumbi huu tumekutana na Maafisa kutoka Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Uhamiaji, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Vyombo hivi vimepewa mamlaka ya kisheria ya kupata taarifa kwaajili ya uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka ya jinai yanayohusu kampuni, lengo ni kuziwezesha kampuni kuongeza uwajibikaji na uwazi katika shughuli zake” amesema Bw. Rweyemamu.

Kwa upande wake Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Bw. Alfredy Mwenda amesema kupitia Sheria hiyo itawawezesha kutambua wamiliki halisi wa kampuni wenye hisa pamoja na Wakurugenzi na kutambua uraia pamoja na vibali vya kuishi na kufanya biashara nchini.

Naye Afisa kutoka TAKUKURU, Bi.Dorothea Kinyonto ameipongeza BRELA kwa mafunzo hayo kwani yanawaongezea ujuzi wa namna kuendesha shughuli zao za kufatilia mambo mbalimbali.

Tunafuatilia mali za watuhumiwa pamoja na utakatishaji fedha katika kampuni mbalimbali, hivyo itatusaidia katika uchunguzi wetu unaohusu ukwepaji kodi kwa kuwafahamu wamiliki halisi wanaonufaika na kampuni”, ameongeza Bi. Kinyonto.

BRELA inaendelea kuratibu na kuwapa elimu wadau mbalimbali kuhusu masuala ya Miliki Manufaa ili Taifa liwe salama katika masuala ya utakatishaji fedha na kufadhili ugaidi.

Mpaka sasa mikoa minne kati ya mitano iliyopangwa kufikiwa imepata elimu hiyo, ambayo ni Dar es salaam, Dodoma, Arusha na Mwanza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!